Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka baba aliyeua binti zake wawili, kujinyonga

17729 Baba+pic TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Siku tatu baada ya mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, Dotusi Isaya kudaiwa kuwaua watoto wake wawili, kumjeruhi kwa panga mkewe pamoja na mama mkwe na kisha kujiua, ndugu wa mwanamke huyo ameibua mapya.

Akizungumza na Mwananchi jana ndugu huyo, Said Mikidadi alisema Isaya hakuwahi kwenda kwao kujitambulisha kama anaishi na ndugu yao kama mke na pia dada yake hakuwahi kwenda kwa ndugu wa mumewe.

Alisema baada ya Isaya kufanya mauaji hayo, juzi waliwasiliana na mwanamke ambaye awali Isaya alimtambulisha kuwa ni mama yake na alipoelezwa kuhusu mauaji hayo alimkana marehemu.

“Tangu alipoanza kuwa na uhusiano na dada amekuja nyumbani mara mbili tu (si kujitambusha), mara ya kwanza ilikuwa wiki mbili zilizopita na mara ya pili ilikuwa ni siku aliyofanya mauaji,” alisema Mikidadi.

Isaya alifanya mauaji hayo usiku wa kuamkia juzi huko Nachingwea mkoani Mtwara. Alikwenda Nachingwea anakoishi mkewe Mariam Lucas na kujificha pembeni mwa nyumba ambayo haijamalizika kujengwa akimvizia kisha kumkata panga eneo la kisogo na begani.

Baada ya tukio hilo Isaya alikwenda katika nyumba (chumba) wanacholala watoto na kuwaua wanawe Clara (5) na Herieth (3), huku akiwaacha watoto wengine wawili waliokuwa wamelala katika chumba hicho.

Katika maelezo yake, Mikidadi alisema watoto hao walizikwa juzi jioni katika makaburi ya Jumuiya kijijini kwao.

“Baba wa watoto hawa (Isaya) mwili wake haujazikwa maana tunaamini ana ndugu zake,” alisema Mikidadi.

Alisema familia yao haikuwa ikimfahamu Isaya kwa kuwa hakuwahi kufunga ndoa na Mariam na walikuwa wakiishi Chanika, Dar es Salaam.

“Mara ya kwanza Isaya alikuja kama wiki mbili zilizopita na kueleza kuwa alikuja kwa lengo la kuwasalimia wanawe lakini hakuondoka kwa ubaya,” alisema Mikidadi.

Alisema mpaka jana, ndugu wa Isaya hawakuwa wamepatikana na walipojaribu kumtafuta, mmoja wa mwanamke ambaye amekuwa akitambulishwa kuwa mama mzazi wa marehemu, alimkana baada ya kuelezwa tukio lililotokea.

“Kulikuwa na mama mmoja ambaye yeye (Isaya) alidai ni mama yake lakini baada ya kupigiwa simu na kuelekezwa matatizo (mauaji) akamkana akasema wanatoka tu kijiji kimoja hamfahamu,” alisema Mikidadi.

“Hata ndugu yetu huyu aliyejeruhiwa (Mariam) kuna matatizo mengine (na Isaya) walikuwa wanaenda kuyasuluhisha kwake (kwa anayedaiwa mama wa Isaya) ila jana ndio kamkataa.”

Alisema Isaya na Mariam walikuwa na migogoro hasa kutokana na dada yake kuwa na watoto wawili, mmoja akiwa mweupe na mwingine mweusi jambo alilodai kuwa Isaya hakulipenda.

Alisema jambo hilo hakuwa akilijua kwa kuwa lilikuwa likifichwa.

“Wale watoto waliouawa mmoja alikuwa mweupe na mwingine mweusi na Isaya alikuwa akisema mtoto mweupe si wake kwa sababu yeye ni mweusi , akawa anamtaka mtoto mweusi (Herieth) baada ya kufarakana,” alisema Mikidadi na kuongeza kuwa ombi hilo lilikataliwa na Mariam kwa kuwa Isaya alikuwa na tabia ya kupiga watoto.

Akizungumzia hali ya Mariam, muuguzi mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, Dk Geofrey Leula alisema Mariam anaendelea vyema na matibabu.

“Anaendelea vizuri na sasa anaweza kuzungumza. Alikuja hapa akiwa hajitambui na alipoteza damu nyingi. Yupo katika maumivu ila tunashukuru anaweza kuzungumza na kutoa taarifa mbalimbali.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pudensiana Protas alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kwa sababu muuaji alijinyonga. “Hatuwezi kumkamata mtu mwingine.”

Watoto wazikwa

Mikidadi alisema watoto hao walizikwa jana jioni.

Alisema kutokana na vifo hivyo kutokea ghafla, hawakuweza kununua majeneza hivyo kulazimika kuwavalisha sanda na kubeba miili yao katika jeneza moja.

Ibada ya mazishi iliongozwa na Katekista kwa Kanisa Katoliki Parokia ya Nachingwea, George Mlanzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz