Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka baba aliyemuua kwa maji ya betri mtoto wake

15098 Pic+batry TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Siku mbili baada ya Geofrey Mwanganga, mkazi wa Kijiji cha Isitu kukamatwa na polisi akituhumiwa kumuua mtoto wake wa miezi mitano kwa kumnywesha maji ya betri, mambo mapya yameibuka.

Mwanganga, ambaye anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi anadaiwa kumnywesha maji hayo ya sumu mtoto wake wa kiume, Prince Godfrey, juzi.

Akizungumzia tukio hilo jana, mwenyekiti wa Kijiji cha Isitu kilichopo wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya, Felix Komba alisema alipokea malalamiko kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Ofisini, Abonike Kajuni aliyemweleza kuhusu kulalamikiwa na mke wa mtuhumiwa huyo.

Komba alisema baadaye alipata maelezo kuwa mke wa Mwanganga aliyemtaja kwa jina moja la Deborah, alifikisha malalamiko kwamba mumewe amemchukua mtoto lakini hajamrudisha na hajui alipo.

Baada ya kupata maelezo hayo, Komba alilazimika kushirikiana na Kajuni kumkasaka na kisha kumkamata mtuhumiwa huyo na kumhoji.

Alisema walipombana aliwaambia kuwa amempeleka mtoto huyo kwa ndugu zake waliopo Iringa mjini.

“Lakini tulipombana zaidi akabadili kauli na kusema amempeleka kwa ndugu zake Igurusi (Mbarali), hapo tukawa na mashaka zaidi tukalazimika kumpeleka Kituo cha Polisi Chimala,” alisema Komba.

Alisema, “kule (polisi) baada ya kuteswa akasema ukweli kwamba amemnywesha maji ya betri kisha akamchukua na kumpeleka porini kumfukia.”

Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kueleza ukweli aliwaongoza maofisa wa polisi, viongozi na majirani hadi alikoufukia mwili wa mtoto huyo.

“Tulikuta mtoto akiwa amefukiwa kwenye shimo na ndipo mwili huo ukachukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Misheni Chimala-Mbarali kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Komba alisema Mwanganga alipoulizwa katika tukio la kuuzika mwili wa mtoto huyo alikuwa na nani, aliwajibu kuwa baada ya kumnywesha maji ya betri alikodi bodaboda hadi porini na kumzika.

“Alisimulia mwenyewe kwamba alipofika porini alishuka kwenye pikipiki kisha akaenda huku akiwa amembeba mtoto huyo bila dereva huyo kujua amebeba nini, na baada ya kutekeleza hilo alirudi alipomuacha mwenzake (dereva bodaboda) kisha wakaanza kurudi kijijini.”

Komba alisema tayari ndugu wamekwishazika mwili wa mtoto huyo baada ya madaktari kuufanyia uchunguzi.

Dada wa Mwanganga, Mary Mndeme alisema kaka yake alikuwa na ugomvi wa muda mrefu na mkewe, ugomvi wao ukihusishwa na wivu wa kimapenzi.

“Kweli kaka yangu alikuwa na mgogoro wa muda mrefu na mke wake, tangu binti akiwa mjamzito hadi amejifungua bado wamekuwa katika hali ya kugombana mara kwa mara,” alisema Mary.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Modestus Chambu alisema wanaendelea kumshikilia Mwanganga huku uchunguzi ukiendelea.

“Unajua kesi za mauaji zina mambo mengi yanahitaji uchunguzi wa kina. Kwa mfano katika hili la kijana huyu kuna mambo ya uchunguzi ikiwezekana kumpima akili, maisha yao (na mkewe) yalikuwaje lakini pia kuna uchunguzi wa kidaktari unasemaje, hivyo tunaendelea nalo kwa mtindo huo kwanza,” alisema.

Katika hatua nyingine, licha ya uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kupokea maelekezo ya amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya kuutoa mwili wa Frank Kapange ili uzikwe, familia ya Kapange imekataa kuuzika na kukata rufaa dhidi ya amri hiyo.

Mwili wa Frank upo mochwari tangu Juni 4 baada ya ndugu kugoma kuuzika wakidai aliuawa na polisi. Mwili huo upo mochwari kwa zaidi ya siku 80. Agosti 24, mahakama hiyo iliamuru mwili huo uchukuliwe na ndugu ili wauzike baada ya kutupilia mbali maombi ya kuiomba iamuru ufanyike uchunguzi wa kiini cha kifo.

Chanzo: mwananchi.co.tz