Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapenzi yahusishwa kifo cha mwanafunzi sekondari

615a026a32eb1b185994da7d086909f6.jpeg Mapenzi yahusishwa kifo cha mwanafunzi sekondari

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWANAFUNZI aliyekuwa akisoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mkolye wilayani Sikonge, Tabora ameuwawa na mwili wake kutupwa vichakani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Safia Jongo alithibitisha kutokea kwa mauaji ya mwanafunzi huyo(jina linahifadhiwa).

"Ni kweli mwanafunzi huyo ameuwawa, sisi Jeshi la Polisi tumefanya upelelezi wa kina na kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na mpenzi wake mmoja ambaye hakumtaja jina lake ambapo baada ya kutengana naye aliamua kutafuta mpenzi mwingine,” alisema Kamanda Jongo.

Baada ya kijana huyo kuona msichana huyo ana mpenzi mwingine alimtishia maisha na huyo msichana akawataarifu wazazi wake lakini hawakutoa taarifa kituo cha polisi Sikonge au katika uongozi kitongoji au wa kijiji.

Kamanda Jongo alisema baada ya mauaji hayo kijana huyo alitoroka kwenda Wilaya ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa na Polisi wanaendelea kumtafuta.

Alisema waliwahoji vijana kadhaa na kuwaachia huru baada ya kubaini hawajahusika na mauaji hayo. Kwa mujibu wa Kamanda Jongo msichana aliuwawa kwa kupigwa na kitu kizito kisogoni.

Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mkolye ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkolye, Elineus Nchimbi alisema tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Kitimbasha katika kata ya Mkolye.

Alisema mwenyekiti wa kitongoji hicho Masulunzu Igoma alimpa taarifa kuwa kuna mwanafunzi alipotea.

Nchimbi alisema baada ya taarifa hiyo siku ya pili wananchi walipewa taarifa na kuanza kumtafuta mwanafunzi huyo, walifanikiwa kuupata mwili katika kitongoji cha Kitimbasha ukiwa vichakani.

Alisema walikuta mwili wa mwanafunzi huyo ukiwa umevuliwa nguo, alikuwa amebakwa na kisogoni alikuwa na jeraha.

Mzazi wa mwanafunzi huyo(jina tunalo) alisema mwanawe aliondoka nyumbani asubuhi akienda shule lakini hakurudi siku hiyo hadi siku ya pili mwili wake ulipookotwa vichakani.

"Nimeumia sana kupoteza mwanangu kwani ameuwawa kikatili sana ila mimi naiomba serikali ifanye uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na unyama huo wa kikatili,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz