Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maofisa watatu Chalinze mbaroni tuhuma za rushwa Sh127 milioni

91255 Pic+takukuru Maofisa watatu Chalinze mbaroni tuhuma za rushwa Sh127 milioni

Thu, 9 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kibaha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kituo maalumu cha Chalinze mkoani Pwani nchini Tanzania imewafikisha mahakamani maofisa watatu wa Halmashauri ya Chalinze kwa tuhuma za kutoa na kupokea rushwa ya Sh127 milioni.

Mbali na maofisa hao waliofikishwa leo Jumatano Januari 8, 2020 Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani pia kuna mkazi mmoja wa Pare kwa makosa hayo.

Waliofikishwa mahakamani ni; Shabani Milao (ofisa mipango wa halmashauri ya Chalinze), Zaina Kijazi (ofisa ardhi wa halmashauri ya Chalinze), Idd Mbato (mwenyekiti wa kitongoji cha Magome na Masoud Kidile ambaye ni mkazi wa kata ya Pera kwa makosa ya kutoa na kupokea rushwa ya Sh127 milioni.

Taarifa ya Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Sadiki Nondo imesema maofisa hao wanatuhumiwa kutenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema makosa hayo yalitendwa kati ya Septemba 25-26, 2019 kitongoji cha Magome Chalinze mkoani Pwani nchini Tanzania.

Nondo amesema washtakiwa hao wamefunguliwa kesi ya jinai Na 10 ya mwaka 2020 katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo. Washtakiwa walisomewa makosa yao mbele ya hakimu wa mahakama ya Mwanzo Chalinze, Rahel Kangakha.

Akisoma  mashitaka hayo, mwendesha mashitaka wa Takukuru, John Sang'wa ameieleza Mahakama washitakiwa wawili Mbato na Kidile wanatuhumiwa kutoa rushwa ya Sh127 milioni kwa nyakati tofauti na kupokelewa na watumishi wa halmashauri ya wilaya Chalinze ambao ni Milao na Zaina Amedai Mbato anadaiwa kiasi cha Sh85 milioni na Kidile anadaiwa kutoa kiasi cha Sh42 milioni ambapo inadaiwa walitoa rushwa hiyo baada ya washitakiwa hao kula njama kwa kuzidisha thamani ya ardhi wakati wa shughuli ya uthamini wa eneo la Magome kata ya Pera Chalinze na kujipatia fedha hizo za ziada zenye thamani ya Sh127 milioni.

“Uthamini huo ulifanywa kwenye eneo lilitwaliwa na Halmashauri ya Wilaya Chalinze kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya mabasi na soko kwa ajili ya wananchi,” amesema Sang'wa

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yanayowakabili.

Kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yana dhamana washtakiwa watatu walipelekwa mahabusu kwa kutokidhi masharti ya dhamana isipokuwa mshitakiwa mmoja Kidile yupo nje kwa dhamana baada  ya kukidhi masharti ya dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz