Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamlaka yachunguza tani ya heroin

39399d0dfa3d6592e86b00958e65ef13 Mamlaka yachunguza tani ya heroin

Mon, 26 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema inachunguza kuhusu mzigo wa dawa za kulevya aina ya heroin uliokamatwa bahari kuu karibu na maeneo ya Kilwa Kisiwani, mkoani Lindi Ijumaa iliyopita.

Mzigo huo unaokadiriwa kuwa zaidi ya tani moja ya heroin ulikamatwa kwa ushirikiano kati ya DCEA, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi.

Watu saba walikamtwa wakiwa na dawa hizo haramu ndani ya meli iliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya uvuvi wa samaki. Kamishina Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya jana alisema mamlaka hiyo imepata mkalimani na inaendelea kuhoji watuhumiwa ambao hawatajwa uraia wao.

Alisema mamlaka hiyo itatoa taarifa baada ya kumaliza kuhoji watuhumiwa hao. Juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Mtatiro Kitinkwi alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya kwenye meli iitwayo Al Arbo.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Amir Hussein, Yusuph Hamad, Salim Mohammad, Ikbal Pakir Mohammad, Jawid Nuhan Nur Mohammad, Mustaphar Nowani Kadirbaksh pamoja na Nahodha wa meli hiyo, Jan Mohammad Miranira.

Alisema mamlaka husika zinaendelea kuchunguza ili kufahamu walikuwa wanatoka nchi gani na walikuwa wakisafirisha mzigo huo kwenda wapi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kilwa ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai alisema meli hiyo ilikamatwa bahari kuu maeneo ya Kilwa Kisiwani Ijumaa saa 2:00 usiku na ililazimishwa kuingia Bandari ya Kilwa.

Alisema wakati wa ukaguzi walibaini kwamba meli hiyo ambayo imetengenezwa kwa ajili ya uvuvi ilikuwa na mzigo mkubwa unaosadikiwa kuwa dawa za kulevya zaidi ya tani moja.

Chanzo: www.habarileo.co.tz