Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama mwenye nyumba adaiwa kumuua dada wa kazi

Mauaji Mlsk Mama mwenye nyumba adaiwa kumuua dada wa kazi

Mon, 13 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ikiwa imezoeleka kuwapo kwa matukio kadhaa ya wasichana wa kazi kutuhumiwa kufanya mauaji, mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Diana Joseph, mkazi wa Tabata Kimanga jijini hapa, anadaiwa kumuua msichana wake wa kazi na kisha kusingizia kuwa alijinyonga.

Diana anatuhumiwa kumuua msichana wake wa kazi za ndani Anne Kassim (20) Februari 8, 2023 saa mbili usiku nyumbani kwake na kisha kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akidai alimkuta binti huyo amejinyonga bafuni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Debora Magiligimba alisema Februari 9 majira ya saa 9:45 asubuhi Jeshi la Polisi walipokea simu kutoka kitengo cha dharura Muhimbili kuhusu mwili huo kufikishwa hospitalini.

“Tulipokea taarifa kutoka kwa mkuu wa kitengo cha dharura kwamba saa 5 akiwa Muhimbili alipokea mwili wa Anne Kasssim akiwa amefariki dunia na uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi ambao ulitufikia ni kwamba alifikwa na umauti baada ya kujinyonga.

“Jeshi lilibaini hapakuwa na dalili zozote za marehemu kujinyonga na mpaka sasa Jeshi la Polisi Ilala, tunaendelea na uchunguzi kuhusu chanzo cha kifo na tunasubiri taarifa za daktari kufahamu kwa kina,” alisema Kamanda Magiligimba.

Kamanda huyo alisema wanamshikilia Diana pamoja na dereva wa taksi mtandao ‘Uber’ ambaye alishirikiana naye kumpeleka Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

Matukio kuhusu wasichana wa kazi

Matukio mengi yamekuwa yakitokea na kuripotiwa yakihusisha wafanyakazi wa ndani kudaiwa kuwaua waajiri wao au watoto wa waajiri wao.

Tukio la karibuni ni la Mhadhiri katika Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) Mwanza Hamida Mussa maarufu ‘Mama Mwakitosi’ kudaiwa kunyongwa na msichana wake wa kazi za ndani.

Mwili wa Hamida ulikutwa nyumbani kwake mtaa wa Buzuruga Mashariki, Novemba 29 mwaka jana. Mtuhumiwa tayari amefikikishwa mahakamani.

Mei 22, mwaka jana, dada wa kazi alidaiwa kumnyonga mtoto Erickson Kimaro mwenye umri wa miaka nane nyumbani kwao Kimara Temboni Dar es Salaam.

Inadaiwa mfanyakazi huyo wa ndani alifika kwenye nyumba hiyo ya mwajiri wake siku ya Jumamosi Mei 28, mwaka jana.

Uongozi wa mtaa, majirani

Mjumbe wa Shina na 11 Kimanga Twiga, Samwel Ilumbi alisema amewahi kupata taarifa za wasichana wa kazi kuteswa katika nyumba hiyo, akitaja simulizi ya binti mmoja aliyelazimika kukimbilia kanisani kupata hifadhi.

“Walinipigia simu nilipofika hali ya binti alikua na makovu ikabidi kama viongozi kwa pamoja tukaamua tumchukue kwa pamoja tukampeleka polisi, lakini ilishindikana baada ya wazazi kushinikiza binti yao arudishwe nyumbani,” alisema mjumbe huyo.

Alisema binti huyo aliyechukuliwa Sumbawanga, alidai kupigwa na kuchanwa na visu pamoja na mapanga.

Kuhusu tukio msichana aliyeuawa, alisema:

“Taarifa tulizonazo huyu binti aliyeuawa kwao ni Biharamuro na kwa maelezo ya mtuhumiwa binti alimkuta amejinyonga kwenye choo. Alipoona akachukua hatua ya kumtafuta dereva wa ubber akamleta wakaubeba mwili na kuupeleka Muhimbili. Madaktari hawakuridhishwa na ndipo wakapiga simu polisi,” alisema Ilumbi.

Askofu wa Kanisa la Pentecostal Congregational Mission, Peter Malembeka alisema Agosti 2022 walimpokea binti anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 19 akiwa na majeraha sehemu mbalimbali ya mwili wake.

“Rekodi ya nyuma kulikuwa na hausigeli anafanya kazi humo ndani. Kwa mujibu wa yule msichana, alikuwa anapigwa kupita maelezo akijeruhiwa na vitu vyenye ncha kali sasa alikimbilia hapa kanisani na sisi kwa mujibu wa maelezo yake tukaona hatutalishughulikia.

“Tukamtafuta mjumbe wa mtaa tukampeleka akajieleza kwa mjumbe tukakubaliana tukaenda mpaka kituo cha polisi alikuwa na makovu akaeleza kwamba anapigwa na mapanga wakati mwingine, huko tukapangiwa siku ya kwenda,’’ alisema askofu huyo ambaye kanisa lake liko jirani na nyumba iliyotokea tukio la mauaji ya msichana huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live