Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama mbaroni ndoa ya mtoto wa miaka 13

Dc94adbba4bda171e4db02c0dd808d16 Mama mbaroni ndoa ya mtoto wa miaka 13

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Polisi mkoani Tabora limekamata watu 10, akiwemo mama mzazi wa binti wa miaka 13 kwa tuhuma za kumuozesha mtoto huyo wa darasa la 7. Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao wakazi wa Manispaa ya Tabora wamehusika kumuozesha binti huyo kwa mwanaume aliyefahamika kwa jina la Abubakar Maulid.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tabora Mjini, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Komanya Kitwala alithibitisha tukio hilo. Alisema kuwa binti huyo alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwanzo katika manispaa hiyo.

Kitwala alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, alifika katika shule hiyo na kuagiza watuhumiwa wakamatwe akiwemo mama mzazi wa binti huyo, Saada Hussein na ndugu waliohusika.

Inadaiwa kuwa baba mzazi wa msichana huyo na shehe aliyefungisha ndoa hiyo, wametokomea kusikojulikana.

Kitwala aliagiza ndoa hiyo ivunjwe na binti arudi shuleni. Aliagiza pia Jeshi la Polisi liwatafute baba mzazi wa binti huyo na shehe aliyefungisha ndoa hiyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwanzo, Salumu Masanja alisema kuwa walimu wa shule hiyo, walikuwa wakijitahidi kumrudisha shuleni mwanafunzi huyo kwa sababu alikuwa mtoro. Kwa mujibu wa walimu hao, jitihada zao zilishindikana kwa kuwa wazazi wa binti huyo walikuwa wakiwatisha.

Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Joel Mkuchika alisema serikali imekuwa ikiwachukulia hatua wazazi wanaokatisha masomo wanafunzi hasa wa kike kwa kuwaozesha na baadhi wamerejeshwa shuleni.

Chanzo: habarileo.co.tz