Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malinzi aiomba mahakama imuachie huru hana hatia

74128 Malinzipic

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumuachia huru kwa sababu hana hatia katika mashtaka 16 yanayomkabili ikiwemo ya utakatishaji fedha.

Pia, mshtakiwa huyo amedai kuwa hakuwahi kushiriki kutakatisha fedha za TFF wala taasisi nyingine maisha yake yote.

Malinzi ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kughushi na kutakatisha fedha, ameieleza mahakama hiyo wakati akijitetea.

Mshtakiwa hiyo ametoa utetezi wake wa saa tano, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Maira Kasonde.

Akiongozwa na Wakili wa utetezi Richard Rweyongeza, mshtakiwa huyo alidai katika mashitaka ya utakatishaji fedha yanaonesha kwamba alitakatisha Sh 43,100,000 kutokana na mashtaka ya kughushi ambayo mahakama hiyo haijamuona kuwa na kesi ya kujibu.

"Sijawahi kushiriki kutakatisha fedha zozote za TFF wala taasisi nyingine katika maisha yangu yote" alidai Malinzi.

Pia Soma

Advertisement   ?
Pia alidai jumla ya fedha zilizoandikwa kwenye mashtaka ya kughushi si Sh 43,100,000 badala yake ni Sh 37,100,000 hivyo idadi iliyowekwa kwenye mashtaka hajui imetokea wapi.

Malinzi alidai fedha anazodaiwa kuzitakatisha alizipata kwa njia halali na zilifuata utaratibu halali wa TFF kwani zipo nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo ikiwemo risiti na nyaraka za benki zinazothibitisha kwamba alipokea fedha kihalali.

"Hadi Desemba 31, 2016 mimi ndio nilikuwa naidai TFF na kwamba kuanzia mashtaka la 15 hadi ya 26 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na sio ya kughushi" alidai Malinzi.

Mshtakiwa huyo, aliendelea kudai kuwa mashtaka ya kughushi aliyonayo hayajaonesha kama alipata kitu chochote kutokana na makosa hayo.

Alidai kuwa alifanya mabadiliko ya mtia saini kutoka Edger Masoud kwenda kwa Nsiande Mwanga kihalali kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba na kanuni za TFF.

Alieleza kuwa si Mamlaka ya kamati tendaji kujadili mtia saini badala yake ni rais ndio anateuwa mtia saini na kupeleka katika bodi ya uamuzi kwa ajili ya kujadili na kisha hupelekwa benki.

"Nilisaini uamuzi ya kubadili mtia saini kwa mujibu wa katiba ya TFF kuonesha kuwakilisha shirikisho, hivyo sikunufaika na kitu chochote kutokana na kubadilisha mtia saini badala yake mabadiliko haya yalinufaisha wengi," alidai Malinzi.

Aliendelea kujitetea kuwa katika muhtasari wa kikao cha Juni 5,2016 uliowasilishwa mahakamani hapo si sahihi na kwamba orodha sahihi ya wajumbe waliohudhuria kikao cha TFF inapatikana kwenye kitabu cha muhtasari na kwamba katika kikao hicho, mashahidi waliokuwepo hawakuhudhuria kikao hicho.

Shahidi ataja fedha za Malinzi Stanbic

Alidai Mwanga hakuhusika kwa namna yoyote kuandaa maamuzi ya bodi na wala hakushiriki katika kufanya maamuzi kwani alikuwa mwajiriwa kama wengine.

Baada ya kusikiliza utetezi huo, hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 13, 2019 kesi hiyo itakapoendelea.

Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mtendaji wa TFF, Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF Nsiande Mwanga na Karani wa TFF, Flora Rauya.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 213/2017, wanakabiliwa na mashitaka 30 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa sababu mashtaka ya utakatishaji fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku Rauya akiwa  nje kwa dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz