Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mali za mamilioni zampeleka kortini ofisa TRA

36867 PIC+MAHAKAMA Mali za mamilioni zampeleka kortini ofisa TRA

Thu, 17 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Summary: Ofisa Msaidizi wa Forodha, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godfrey Mapuga, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la kumiliki mali zenye thamani ya Sh721 milioni zisizoendana na kipato chake cha sasa na cha zamani.

Dar Es Salaam. Ofisa Msaidizi wa Forodha, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godfrey Mapuga amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka moja la kumiliki mali za thamani ya Sh 721 milioni ambazo haziendani na kipato chake cha sasa na cha zamani.

Mapunga anadaiwa kumiliki viwanja vitatu pamoja na nyumba moja ya ghorofa, ambavyo haviendani na kipato chake.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Vitalius Peter akisaidiana na Lilian William amedia leo Januari 15, 2019 mbele ya Hakimu Mwandamizi, Salum Ally, kuwa mshtakiwa anakabiliwa shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 13/2019.

Akimsomea shtaka hilo, wakili Lilian alidia kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya April Mosi, 2011 na Julai 19, 2016 eneo la  Ubungo.

Alidai kuwa, Mapuga akiwa kama mtumishi wa umma, anadaiwa kumiliki nyuma moja ya ghorofa, iliyopo Goba Manispaa ya Ubungo, yenye thamani ya Sh 698,921,217, ambayo haiendani na kipato chake cha sasa na cha zamani.

Wakili Lilian alidai katika kipindi hicho, Mshtakiwa anadaiwa kumiliki kiwanja kimoja ambacho hakijasajiliwa kilichopo eneo la Mbezi Juu, Manispaa ya Ubungo chenye thamani ya Sh7 milioni.

Pia, anadaiwa kumiliki ardhi ambayo haijasajiliwa iliyopo eneo la Kigamboni, yenye thamani ya Sh 6milioni.

Mapuga anadaiwa kumiliki kiwanja ambacho hakijasajiliwa kilichopo Goba, chenye thamani Sh 9.5miloni na kufanya idadi ya mali anazodaiwa kumiliki ambazo haziendani na kipato chake cha sasa na cha zamani kufikia Sh721,421,217.

Mshtakiwa ambaye anatetewa na Wakili Mluge Fabian, baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, alikana kutenda kosa hilo.

Wakili Peter alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba terehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali (PH).

Hakimu Ally, alitaja masharti matano ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo. Sharti ya kwanza, mshtakiwa anatakiwa awasilishe fedha taslimu kiasi cha Sh360,710,608 au mali  isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Pia mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini dhamana ya ahadi kila mmoja ya Sh360,710,608.

Masharti mengine ni mshtakiwa kutoruhusiwa kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama, kuwasilisha hati yake ya kusafiria Mahakamani na kuhudhuria kesi yake kila inapotajwa.

Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kirudishwa rumande huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Januari 29, 2019.



Chanzo: mwananchi.co.tz