Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makosa manne yamfikisha Mwalimu Mkuu kizimbani

Wee Jail Makosa manne yamfikisha Mwalimu Mkuu kizimbani

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mwanangwa Baraka Mwansasu(34) iliyoko wilayani Misungwi mkoani Mwanza amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Misungwi akishitakiwa kwa makosa manne la rushwa na matumizi mabaya ya mamlaka, ubadhirifu na ufujaji wa mali.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Saida Salum mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Erick Marley kwamba Mwalimu Mwansasu alifanya kosa la kughushi nyaraka kinyume na kifungu cha pamoja na kosa la kuwasilisha nyaraka za uongo.

Salum aliieleza mahakama hiyo kuwa mwaka 2018 shule ya Msingi Mwanangwa iliingiziwa fedha kwenye akaunti yake na Wizara ya Elimu kiasi cha Sh 2,000,000 kwa ajili ya motisha kwa walimu kwa madai kuwa mwaka 2017 shule hiyo ilifanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba.

Alisema hata hivyo kutokana na uchunguzi uliofanywa na Takukuru wilaya ya Misungwi ulibaini kuwa baada ya Wizara kuingiza fedha hizo katika kipindi cha mwaka 2018 Mwalimu Mwansasu akiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mwanangwa aligushi muhtasari wa Kamati ya Shule na kuuwasilisha kwa Ofisa Elimu Kata na Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Misungwi kwa lengo la kuonesha kuwa Kamati ya shule ilikaa na kuidhinisha kutolewa kwa kiasi hicho cha fedha Sh 2,000,000 ili ziweze kutumika.

Aliongeza kuwa baada ya kutimiza lengo lake hilo huku akijua kuwa anachokifanya ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi, alifanikiwa kutoa fedha hizo na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, mtuhumiwa alikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Marley na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana aliyotakiwa kuwa wadhamini wawili na kila mmoja alisaini bondi yenye thamani ya Sh 1,000,000 masharti ambayo aliyatimiza.

Aidha kufuatia kutimiza masharti ya dhamana, kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 25 mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Chanzo: habarileo.co.tz