Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makarani wa TPA kortini wizi wa madini ya mil 700/-

85ca7d713e02f6aa5a7ecb5ed55b476f.jpeg Makarani wa TPA kortini wizi wa madini ya mil 700/-

Sat, 10 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU sita, wawili wakiwa ni makarani wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka matano likiwamo wizi wa madini aina ya tantalite yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 700.

Frank Julius na Majiba Konga ambao ni makarani wa TPA pamoja na wengine wanne, walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid.

Washitakiwa wengine wanaodaiwa kutenda makosa hayo Februari 23, mwaka huu katika eneo la TPA, ni Usemali Ichimulyabe na Ali Jadil (walinzi), Peter Michael (dereva) na Patrick Malwa ambaye ni mfanyabiashara.

Akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali, Nguka Faraji alidai walitenda makosa hayo Februari 23, mwaka huu TPA, Temeke, Dar es Salaam ambako walikula njama za kutenda uhalifu na kisha kughushi nyaraka kufanikisha wizi wa madini hayo.

Wanadaiwa kughushi risiti ya kusafirisha, kibali cha kupitisha na waraka wa kuhamisha mzigo huo kutoka bandarini kwenda bandari kavu.

Mwendesha mashitaka alidai kuwa Februari 23, mwaka huu waliiba tani 10,443.05 za madini aina ya tantalite yenye thamani ya Sh 789,285,429.53 mali ya Kampuni ya Novacole FZE yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Rwanda kwenda Falme za Kiarabu.

Washitakiwa wote walikana mashitaka. Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 27, mwaka huu na washitakiwa wote walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kwa kila mmoja watakaosaini bondi Sh milioni 100 na mdhamini mmoja au wote wawasilishe hati ya mali isiyohamishika ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Chanzo: www.habarileo.co.tz