Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makandege wa ITPL apandishwa kortini, akosa dhamana

89410 IPTL+PIC Makandege wa ITPL apandishwa kortini, akosa dhamana

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kujipatia fedha kiasi cha dola za kimarekani 980,000 kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Dola za kimarekani 980,000.

Makandege amefikishwa mahakamani hapo, leo Ijumaa Desemba 20, 2019 na kusomewa mashtaka yake mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Faraja Nchimbi na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27/ 2017.

Makandege ambaye anatetewa na wakili Joseph Sungwa ameunganishwa na wenzake wawili katika kesi hiyo ambao ni Harbinder Seth, ambaye alikuwa Mwenyekiti Mtendaji wa PAP na Mkurugenzi wa VIP Solution, James Rugemarila.

Mshtakiwa huyo ameunganishwa na wenzake, baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo kumuunganisha mshtakiwa huyo.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili Kadushi amedai katika shtaka la kwanza, Makandege anadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India alikula njama za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Vile vile, mshtakiwa huyo anadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya dola za Kimarekani 980,000 ambapo kosa hilo anadaiwa kulitenda kati ya Januari 23, 2014 na Februari 10, 2014 katika benki ya Stanbic iliyopo wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam nchini Tanzania  na UBL bank(T) Ltd, iliyopo wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, wakili Nchimbi alidai, kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014 katika benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na benki ya UBL bank(T) Ltd iliyopo wilaya ya Ilala, mshtakiwa kwa nia ya ulaghai, alijipatia fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania kiasi cha dola za kimarekani USD 380,000 na dola za kimarekani USD 600,000.

Mashtaka mengine yanayomkabili mshtakiwa huyo ni kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa na kutakatisha fedha kiasi cha dola za kimarekani USD 980,000 kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake, hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi, Januari 2, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande na mshtakiwa amerudishwa rumande kutoka na mashtaka ya kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz