Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makandege wa IPTL abadilishiwa mashitaka

Makandepeicc Makandege wa IPTL abadilishiwa mashitaka

Fri, 22 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mwanasheria wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege umesema bado hawajafikia muafaka wa mazungumzo baina yao na mshtakiwa huyo.

Makandege anayekabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 980,000, ameomba kufanya majadiliano na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) ili kukiri kosa.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kutoa mrejesho wa majadiliano ya mazungumzo ya awali, ambapo hawajafikia muafaka wa mazungumzo baina yao.

Oktoba 20, 2021 Makandege aliomba tena kufanya mazungumzo na DPP kufanya majadiliano ya kukiri makosa yanayomkabili ili kupata nafasi ya kwenda kushiriki msiba wa baba yake mzazi.

Komanya amedai kuwa baada ya kutafakari DPP ameridhia kufanya mabadiliko katika hati ya mashtaka hivyo, kurekebisha kifungu cha 234(1) cha sheria ya mwenendo wa jinai.

"Kwamba mabadiliko hayo katika mashtaka aliyokuwa akikabiliwa limetolewa la utakatishaji wa fedha na kubakisha mengine yote hivyo, tunaomba kukabidhi hati ya mabadiliko haya kwenye mahakama hii," alidai Komanya.

Baada ya wasilisho hilo, Komanya alimsomea upya mshtakiwa hiyo mashtaka yanayomkabili ambalo ni la kuongoza genge la uhalifu, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara.

Komanya alidai katika shtaka la kwanza inadaiwa kuwa alitenda kosa hilo kati ya Oktoba 18,2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, ambapo Makandege alikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka hilo ambalo ni la kuongoza genge la uhalifu, Makandege anadaiwa kutenda kosa hilo katika nchi hizo, na kwamba akiwa si mtumishi wa Serikali alishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango huo wa uhalifu.

Katika shtaka la pili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Makandege anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014.

Kwamba alijipatia dola 380,000 katika benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na dola 600,000 katika benki ya UBL Bank (T) Ltd iliyopo wilayani Ilala, fedha zilizotoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa nyakati tofauti.

Shtaka la mwisho ni la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000, ambapo Komanya alidai kuwa upelelezi bado haujakamilika hivyo, aliiomba mahakama hiyo iwapangie tarehe nyingine ya kutajwa wakiwa kwenye muda wa mazungumzo.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi hivyo, kama mshtakiwa anataka dhamana basi aende Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka.

Chanzo: mwananchidigital