Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makandege wa IPTL aachiwa kwa dhamana

Makandegepic Makandege wa IPTL aachiwa kwa dhamana

Wed, 27 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mwanasheria wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege ameachiwa kwa dhamana leo Jumatano Oktoba 27, 2021.

Makandege anayekabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 ametoka nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti yaliyotolewa na Mahakama Kuu.

Mahakama Kuu ilimtaka Makandege awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi pamoja na hati yenye thamani ya kiasi cha nusu ya fedha aliyoisababishia hasara Serikali.

Pia mahakama hiyo imemtaka mshtakiwa kutosafiri nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali pamoja na kuwasilisha hati ya kusafiria.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Faraji Nguka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya dhamana.

Nguka alidai kuwa kama mshtakiwa huyo atakuwa ametimiza masharti ya dhamana aliyopewa na Mahakama kuu ya Tanzania hakutakuwa na pingamizi.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi aliwauliza upande wa utetezi kama wanalipa fedha taslimu au mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi cha nusu ya fedha aliyoisababishia Serikali hasara.

Alex Balomi aliieleza mahakama hiyo kuwa watatoa hati ya nyumba yenye thamani ya kiasi cha fedha cha Sh784 milioni.

"Sisi tumekamilisha masharti ya dhamana kama ilivyopangwa na Mahakama kuu ya Tanzania" Balomi.

Chanzo: mwananchidigital