Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ataka wananchi kusaidia kuwabaini wahamiaji haramu

39e2ab9c9cec1b7c9c4074ca9fbd9210 Majaliwa ataka wananchi kusaidia kuwabaini wahamiaji haramu

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa idara ya uhamiaji katika kutoa taarifa za viashiria vya uingiaji wa wahamiaji haramu ili waweze kudhibitiwa kabla hawajaingia nchini.

Alitoa ushauri huo alipotembelea kambi ya mafunzo kijeshi ya Uhamiaji iliyopo eneo la Bomakichakamiba wilayani Mkinga ikiwa ni mwishoni mwa ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo na uhamasishaji wa kilimo cha mkonge mkoani Tanga.

Alisema kuwa mkoa wa Tanga umekuwa ni miongoni mwa mikoa yenye changamoto ya uingiaji wa wahamiaji haramu hivyo aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa kituo hicho ili waweze kudhibitiwa.

“Wananchi tusaidie kuwaibua wahamiajj haramu kwani jeshi la Uhamiaji limekuwa likifanya jitihada kubwa katika kukabiliana na udhibiti wa wahamiaji haramu hao” alisema Waziri Mkuu .

Alisema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kuimarisha miundombinu ya majeshi yetu ikiwemo maeneo ya kufanyiakazi ili kuboresha ufanisi wa ufanyajikazi wao.

“Napenda niwahakikishe serikali yenu itaboresha mazingira ya kambi hii ili iiendane na hadhi ya utoaji wa mafunzo hayo ikiwemo kitaifa na kimataifa” alisema Waziri Mkuu.

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani, Hamis Hamza Hamis alisema kuwa uwepo wa kambi hiyo ni sehemu ya manufaa kwa wananchi wa maeneo ya jirani kwani watapata fursa ya kupata huduma za jamii kwa urahisi.

Kamishna wa uhamiaji nchini , Dk Anna Makakala alisema kambi ya Boma Kichakamiba ina jumla ya wanafunzi 287 wanawake wakiwa ni 81 na wanaume ni 206.

Chanzo: habarileo.co.tz