Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaji watoa somo kwa mahakimu kuhusu Utakatishaji Fedha

LU16 Jaji wa Mahakama Kuu , Awamu Mbagwa akielezea kosa la utakatishaji fedha

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mafunzo ya kuwajengea uwezo na uelewa Mahakimu Wakazi 200 yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yameingia siku ya pili ambapo Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania wamewapitisha washiriki kwenye mada kuu mbili muhimu zinazohusu utakatishaji fedha na urejeshaji mali zinazopatikana kwa njia ya uhalifu.

Mmoja wa Majaji hao, Awamu Mbagwa amewaeleza Mahakimu hao kwa kina hatua zinazochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania kupambana na makosa ya uhalifu wa kifedha kwa kuzingatia athali ambazo hutokea kijamii, kisiasa na kiuchumi. Majaji wengine walioshirikiana naye katika kuwawezesha washiriki hao ni Edwin Kakolaki na Dkt. Zainab Mango.

Akizungumzia kosa la kutakatisha fedha, Mbagwa amesema kuwa utakatishaji fedha ni namna ya kujipatia fedha haramu, fedha ambazo hutokana na uhalifu na kutafuta njia mbalimbali kuwezesha fedha hizo zionekane kuwa ni halali.

Kwa mujibu wa Jaji Mbagwa, mtu anaweza kupata fedha haramu, lakini ili kuzihalalisha anaamua kuziwekeza ama kwa kununua hisa, kujenga nyumba au kuziingiza kwenye uwekezaji wowote wa kibiashara au viwanda, lengo likiwa kuonyesha uwekezaji huo ni halali, huku akijua chanzo cha fedha hizo ni haramu.

Amesema kuwa hapo awali chimbuko la kosa hilo lilikuwa ni kujihusisha na dawa za kulevya. Hata hivyo, Jaji Mbagwa amebainisha kuwa mabadiliko kadhaa yalifanyika ili kupanua uwigo wa kupambana na athali zinazotokana na kosa hilo na kujumuisha makosa yote ya uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, juhudi ambazo zililenga kuwashughulikia wote wanaonufaika na mazao yanayotokana na makosa tangulizi kwa vile ilikuwa vigumu kuwapata mapapa wa uhalifu wanaojihusisha na makosa hayo.

“Ili kuendana na matakwa ya sheria za kimataifa, Tanzania ilitunga sheria ya utakatishaji fedha mwaka 2006. Kwa mujibu wa sheria hii, utakatishaji fedha ni kosa linalosimama pekee yake bila mtu kushitakiwa kwanza na makosa mengine tangulizi. Kwa hiyo, siyo lazima kuthibitisha kosa tangulizi ili kumtia hatiani mtu kwenye kosa la utakatishaji fedha,” amesema.

Sheria hiyo imebainisha makosa mbalimbali ya utakatishaji wa fedha, ikiwemo mtu yeyote atakaye jihusisha, moja kwa moja au kwa njia nyingine katika muamala unaohusisha mali itokanayo na mapato ya fedha haramu akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu mali hiyo ni mazao yatokanayo na makosa ya uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu.

Kwa mujibu wa sheria hii, kosa jingine ni mtu yeyote atakaye badili, hamisha, safirisha, pitisha mali ikiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo ni ya mapato yatokanayo na uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu, kwa malengo la kuficha, kupoteza ukweli au chanzo halisi cha mali hiyo kuwa ni haramu au kumpa msaada mtu yeyote aliye husika katika kufanya kitendo hicho kwa lengo la kukwepa madhara ya kisheria.

Kosa jingine ni pale mtu yeyote atakaye ficha, funika ukweli, zuia upatikanaji wa ukweli, chanzo,mahali,Uhamishaji wa umiliki, mzunguko, au umiliki wa au haki kuhusiana na mali hiyo, akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo imepatikana kwa mapato yatokanayo na fedha haramu.

Amebainisha pia kuwa ili kuweza kupambana na makosa hayo ya uhalifu wa kifedha mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania, yaliamua kuanzisha sheria ili kukamata mali zote zinazopatikana kwa njia za kihalifu, malengo yakiwa kuondoa motisha zainazotokana na uhalifu huo na pia kuzuia wahalifu kufanya uhalifu zaidi

Chanzo: www.tanzaniaweb.live