Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaji wanne kusikiliza rufani 29 kwa wiki tatu

B728ed5553ee92b12e764244c90bebdb Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis

Tue, 19 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Jopo la majaji wanne wa Mahakama ya Rufaa Tanzania limeanza kusikiliza mashauri ya rufaa 29 katika Mkoa wa Mara na wataifanya kazi hiyo kwa wiki tatu.

Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma jana alizindua usikilizwaji wa rufaa hizo mjini hapa. Majaji wengine watakaoifanya kazi hiyo ni Jaji Ferdinand Wambali, Jaji Ignas Kitusi na Jaji Lilian Mashaka.

Akizungumza kabla ya ufunguzi wa vikao hivyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Musoma, Jaji John Kahyoza alisema awali wananchi walifuata huduma hiyo jijini Mwanza.

Msajili wa Mahakama ya Rufani, Kervin Mhina alisema rufaa hizo zinafanyiwa kazi na vikao vilianza jana mpaka Novemba 5 mwaka huu, ambapo 17 ni za jinai, 10 za madai na maombi mawili.

Kahyoza alisema mpaka sasa kuna mashauri 321 yanayohitaji kufanyiwa kazi katika Mahakama ya Rufani, kati ya hayo 171 ni ya jinai, 132 ya madai na manane ya maombi.

"Mheshimiwa Jaji Mkuu tukirejea utaratibu wa vikao hivi kufanywa mara moja kila mwaka, inamaanisha ili kumaliza mashauri tuliyonayo itatuchukua siyo chini ya miaka 10," alisema.

Kahyoza alimuomba Profesa Juma kuona uwezekano wa kuongeza idadi ya vikao hivyo kwa mwaka au kuongeza majopo ya majaji ili kazi imalizwe mapema na kwa ufanisi.

Akizungumza kabla ya kufungua rasmi vikao hivyo, Jaji Mkuu Juma aliahidi kufanyia kazi ombi la kuongeza vikao au majopo ya majaji katika mahakama hiyo ili kukidhi mahitaji.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa jengo la Mahakama Kuu limefungwa mitambo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), mashauri yanaweza kusikilizwa hata bila ya majaji kwenda Musoma.

Profesa Juma alitaka jengo hilo liwe sehemu ya kituo cha taarifa kwa wananchi kwa lengo la kuwezesha kupatikana suluhu na upatanishi badala ya kila shauri kufikishwa mahakamani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz