Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaji wabariki kifungo cha maisha kwa msafirishaji wa mirungi

13901 Mirungi+pic TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ‘wamebariki’ kifungo cha maisha jela alichohukumiwa mkazi wa Moshi, Slahi Jumanne kwa kusafirisha kilo 21 za mirungi.

Jopo hilo lililoundwa na majaji Mbarouk Salim Mbarouk, Dk Gerald Ndika na Jacob Mwambegele limekubaliana na hoja zilizowasilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme.

Hukumu ya kifungo cha maisha ambayo ilikuwa ya kwanza tangu kuundwa kwa taifa la Tanzania katika kesi ya kusafirisha mirungi ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari, Machi, 2016.

Baada ya kutolewa hukumu hiyo na gazeti hili kuiripoti, kuliibuka mijadala ndani na nje ya nchi, baadhi ya watu wakihoji inakuwaje anayepatikana na hatia ya usafirishaji mirungi afungwe kifungo cha maisha.

Hata hivyo, mfungwa huyo alikata rufani Mahakama ya Rufaa Tanzania akipinga adhabu hiyo, lakini jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo wamesema kifungo hicho kilikuwa sahihi.

Katika hukumu yao hiyo ambayo Mwananchi limeona nakala yake, majaji hao watatu wamesisitiza kuwa hawakuona dosari zozote katika kifungo cha maisha alichopewa mtuhumiwa huyo, hivyo aendelee nacho.

“Mtu anayekiri kwa hiyari yake kutenda kosa la jinai (kama Slahi Jumanne alivyokiri kosa hilo katika maelezo yake) ni shahidi bora katika shitaka analokabiliwa nalo,”wamesema majaji hao.

“Katika uchambuzi wa mwisho tunaona hakukuwa na dosari katika kutiwa hatiani kwa mrufani na pia adhabu ya kifungo cha maisha alichopewa kwa sababu ndio adhabu ya kosa hilo,”walisisitiza.

Katika usikilizwaji wa kesi mbele ya Jaji Sumari, upande wa mashtaka ulioongozwa na wakili Tamari ulidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 7, 2013 katika Manispaa ya Moshi.

Wakili Tamari ambaye alisaidiana na wakili wa Serikali, Kassim Nasir alidai siku hiyo katika kituo kikuu cha mabasi Moshi, mshtakiwa alikamatwa na dawa hizo zenye thamani ya Sh1,050,000.

Katika hukumu yake, Jaji Sumari alisema mashahidi watano wa upande wa mashtaka, wamethibitisha kuwa mshtakiwa alikamatwa na begi la rangi ya kijani likiwa na mirungi hiyo.

Alisema licha ya mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na Wakili Martin Kilasara kujitetea kuwa hakukamatwa Stendi Kuu bali eneo la Majengo mjini Moshi, ushahidi umethibitisha alikamatwa Stendi Kuu.

“Baada ya kusikiliza, mashahidi wamethibitisha ulikamatwa Stendi Kuu Moshi, ushahidi huo uliungwa mkono na kondakta wa basi na dereva teksi aliyekuchukua,” alisema.

Jaji alisema polisi hawakuwa na sababu yoyote ya msingi ya kumbambikia shtaka mshtakiwa huyo kama alivyojaribu kujitetea na kusisitiza kuwa ushahidi ulikuwa madhubuti dhidi yake.

“Kulikuwa na tofauti ndogondogo kama begi lilibebwa na nani kutoka stendi au kutoka kwenye basi hadi kwenye teksi. Zilikuwa ni tofauti ndogo hazikuharibu mizizi mikuu ya ushahidi,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Sumari, ukiacha ushahidi huo, ungamo la mshtakiwa la kukiri kosa hilo alilolitoa kwa hiyari yake linaongeza nguvu na kushabihiana na ushahidi uliotolewa na mashahidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz