Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majadiliano DPP, bosi Jatu Saccos hayajakamilika

Jatu Picsss Majadiliano DPP, bosi Jatu Saccos hayajakamilika

Tue, 21 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema inaendelea na majadiliano ya maridhiano ya kukiri kosa katika kesi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya.

Gasaya (33), anakabiliwa na makosa mawili katika kesi ya uhujumu uchumi, akidaiwa kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai kuwa atazipanda kwenye kilimo ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua ni uongo.

Akizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Mei 21, 2024 Wakili wa Serikali, Eva Kassa, kesi ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini amesema wameanza vikao kati ya mshtakiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

"Tumeanza vikao vya Plea Bargaining (mkataba wa maridhiano kukiri kosa) baina ya mshtakiwa na DPP, bado hatujafikia hitimisho, leo tulitakiwa kuendelea na vikao lakini wakili wa Gusaya, Nafikile Mwambombo yupo Mahakama Kuu kwenye kesi nyingine, kwa sababu hiyo tunaomba kesi hii ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na pia kuendelea na vikao vya majadiliano," ameomba wakili Kassa.

Hakimu Mhini amekubali kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 3, 2024 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua iliyofikiwa katika majadiliano.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shitaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Machi 12, 2024, Gusaya alimwandikia barua DPP kukiri kosa na kuomba apunguziwe adhabu.

Kutokana na barua hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa Gusaya kuanza majadiliano na DPP.

Katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi namba 8/2023 anashitakiwa kwa makosa mawili, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, na kutakatisha Sh5.1 bilioni.

Katika shitaka la kwanza, anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh 5.139 bilioni kutoka Saccos ya Jatu akidai fedha hizo atazipanda kwenye kilimo, jambo ambalo alijua siyo kweli.

Shitaka la pili anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha, kosa analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa kujihusisha na muamala wa kiasi hicho cha fedha kutoka akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda akaunti ya Jatu PLC iliyopo katika tawi hilo, akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live