Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maimu wenzake wafutiwa mashtaka 10

1449d39fd08f8c8e237d4da70afc02dd Maimu wenzake wafutiwa mashtaka 10

Sat, 23 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dickson Maimu na wenzake, wamefutiwa mashtaka 10 ya utakatishaji wa fedha

Mbali na Maimu washitakiwa wengine waliofutiwa mashitaka hayo ni aliyekuwa Ofisa Usafirishaji Nida, George Ntalima na Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Awali washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka 55 likiwamo utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 1.175

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya amedai leo Oktoba 22 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa lakini wanakusudia kufanya mabadiliko katika hati ya mashtaka.

Amedai kesi hiyo iko katika hatua za usikilizwaji na kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) amekusudia kufanya marekebisho madogo chini ya kifungu cha 234(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA).

Jumla ya mashtaka yaliyokuwa yanawakabili ni 55, baada ya marekebisho hayo yatakuwa mashtaka 45, kwa mshtakiwa wa kwanza Dickson Maimu, mshtakiwa wa tatu, George Ntalima na wa nne Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo ambao wameondolewa mashtaka ya utakatishaji fedha.

Wakili Komanya amedai endapo hakutakuwa na pingamizi, wangeomba kuwasilisha hati mpya, hata hivyo hati hiyo haikupokelewa kutokana na Hakimu Mkazi Mkuu Rashid Chaungu anayesikiliza kesi kutokuwepo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 4 mwaka itakapotajwa ambapo upande wa mashtaka utawasilisha hati mpya.

Katika kesi hiyo, tayari upande wa mashitaka umeshafunga ushahidi kwa kuwaita jumla ya mashahidi 26 pamoja na kuwasilisha vielelezo 45.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Meneja Biashara wa (Nida), Aveln Momburi na Mkurugenzi wa Sheria, Sajina Raymond.

Chanzo: www.habarileo.co.tz