Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maimu, wenzake wafutiwa mashitaka, wakamatwa tena

38844 MAIMU+PIC Maimu, wenzake wafutiwa mashitaka, wakamatwa tena

Thu, 31 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewafutia mashtaka aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake sita.

Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao leo Jumatatu Januari 28, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.

Maimu na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka zaidi ya 20 yakiwemo ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1.1 bilioni.

Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Wakili wa Serikali Simon Wankyo akisaidiana na Leonard Swai, amedai mbele ya Hakimu Mtega kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Wankyo amedai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao ambako hakimu Mtega alisema kutokana na maombi hayo, mahakama imeifuta kesi hiyo.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja biashara wa (Nida), Avelin Momburi na mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani.

Wengine ni mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, ofisa usafirishaji, George Ntalima, mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kufutiwa kesi hiyo na kutoka katika chumba cha mahakama, walikamatwa na kupelekwa mahabusu na kisha wakatolewa na kupandishwa katika gari la Takukuru na haijajulikana wanapelekwa wapi.

:Soma zaidi >>Upelelezi kesi ya vigogo wa Nida haujakamilika

                     >>Mshtakiwa kesi ya Maimu afariki dunia



Chanzo: mwananchi.co.tz