Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amesema Mahakama Maalumu za udhalilishaji wa kijinsia zimeanza kwa kasi.
Abdalla amesema hayo wakati alipokutana na balozi wa Ireland nchini, Mary O’Neal, Vuga mjini Unguja ambapo mazungumzo yao yalilenga katika kuboresha sekta ya sheria nchini.
Alisema kwa muda mrefu makundi mbalimbali ya kijamii yalikuwa na malalamiko kuhusu kuchelewa kusikilizwa kwa kesi za udhalilishaji wa kijinsia lakini katika miezi sita mahakama imefanyakazi kubwa.
Alikiri kuwepo kwa msongamano wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia ambazo zimechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kukamilika kwa upelelezi na jamii yenyewe kukataa kutoa ushirikiano wakati wa utoaji ushahidi mahakamani.
Aidha, sababu nyingine ni kuwa na majengo finyu kama ilivyo kwa Mahakama ya Vuga ambayo inakabiliwa na uhaba wa nafasi kuanzia vyumba vya kusikiliza kesi za wananchi pamoja na ofisi kwa mahakimu na majaji.
“Tumeanza kusikiliza kesi za udhalilishaji kwa kasi kubwa kiasi cha kuanzisha Mahakama maalumu za wa kijinsia na hivyo kuleta matokeo mazuri ambapo hukumu mbalimbali za kesi za kubaka zenye kifungo kuanzia miaka 13- hadi 30 zimetolewa,’’ amesema.