Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yawatahadharisha upande wa mashataka wasipoleta mashahidi

HUKUMU Mahakama yawatahadharisha upande wa mashataka wasipoleta mashahidi

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema upande wa Jamhuri wasipoleta mashahidi tarehe ijayo katika kesi inayowakabili washtakiwa 12 wakiwemo walimu itatoa uamuzi kwa mujibu wa sheria inavyotaka.

Hatua hiyo imekuja leo Agosti 21, 2023 baada Wakili wa upande wa Utetezi, Nestory Mkoba kuieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo limekuwa likiahirishwa mara kwa mara bila ya kuletwa mashahidi.

"Julai 24, 2023 mahakama yako tukufu iliwapa onyo mashahidi wawili maana yake hadi wanafika mahakamani upelelezi ulishakamilika hadi iweje leo hii upande wa mashtaka wanatuambia jalada limeitishwa polisi kwa ajili ya uchunguzi sisi tunaona hawana nia ya kuendelea na shauri hili,"amedai Mkoba.

Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo amesema anaungana na upande wa utetezi kwa kuwa shauri hilo ni la muda mrefu hivyo upande wa Jamhuri wasipoleta mashahidi tarehe ijayo mahakama hiyo itatoa uamuzi kwa mujibu wa sheria inavyotaka.

"Hili ni ahirisho la mwisho hakikisheni tarehe ijayo upande mashtaka mnaleta mashahidi msipofanya hivyo mahakama hii itatoa uamuzi wake," amesema Mazengo.

Awali, Wakili wa Serikali, Titus Aron alidai alidai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya usikilizwaji lakini jarada limeitishwa polisi kwa ajili ya uchunguzi.

"Hatuwezi kuendelea kwa kuwa hawana jarada lipo polisi hivyo tunaiomba mahakama hii iahirishe shauri hili itupe siku 14 tuweze kuendelea, "amedai Aron.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa ushahidi Septemba 11, 12 na 13, 2023.

Washtakiwa hao ni Jahnson Ondieka (37), Patrick Chawawa, Theresia Chitanda, Elinami Sarakikya, Joyce Nyanyakila na Gladius Roman, Dorcas Muro, Alcheraus Malinzi, Jacob Adagi na Joel Ngome.

Inadaiwa kati ya Oktoba 2, 2022 na Oktoba 12, 2022 sehemu isiyojulikana mshtakiwa Malinzi akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo wa mtihani wa somo la uraia la darasa la saba akijifanya mtihani huo ni halali na umeandaliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Pia, tarehe hiyo na sehemu isiyojulikana mshtakiwa Malinzi akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo wa mitihani wa somo la Maarifa ya Jamii wa darasa la saba uliojifanya mwaka 2022, alionyesha kuwa mtihani huo umeandaliwa na Necta.

Katika shtaka la tatu, mshtakiwa Adagi na Ngome wanakabiliwa na shtaka moja la kuvujisha mitihani ya Taifa ya darasa la saba, kinyume cha sheria.

Chanzo: mwanachidigital