Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yawaonya wabunge wanne wa Chadema

85132 Msigwa+pic Mahakama yawaonya wabunge wanne wa Chadema

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaonya wabunge wanne wa Chadema waliokiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani bila taarifa yoyote.

Onyo hilo limetolewa leo Jumatano Novemba 20, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kusikiliza utetezi wao, kubainisha kuwa haukujitosheleza lakini hatowafutia dhamana kwa kuwa itakuwa hatua kali.

Novemba 15, 2019 mahakama hiyo iliamuru wabunge hao, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); John Heche (Tarime Vijijini); Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda) kukamatwa baada ya siku hiyo kukiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.

Mbali na kutoa amri hiyo, mahakama hiyo pia ilitoa hati ya wito kwa wadhamini  wao kujieleza kwa nini  hawakuwapeleka washtakiwa  mahakamani.

Wabunge hao walianza kujisalimisha kuanzia Jumamosi iliyopita na leo mahakama hiyo ilipanga kutoa uamuzi kuhusu kukiuka kwao dhamana.

Wabunge hao pamoja na wenzao watano akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Akitoa uamuzi huo Hakimu Simba amesema maelezo yaliyotolewa na washtakiwa hao pamoja na wadhamini wao hayajitoshelezi lakini kuwafutia dhamana ni hatua kali.

Amesema washtakiwa hao kujisalimisha polisi walikuwa wakiogopa kitakachowapata.

Ijumaa iliyopita Mbowe,  katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na Esther Matiko (Tarime Mjini) ndio waliofika mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz