Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yatupa pingamizi la mtoto wa Mwakipesile

Mahakama Pic Mahakama yatupa pingamizi la mtoto wa Mwakipesile

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkazi Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imetupilia mbali pingamizi la Boniface Mwakipesile aliyeiomba mahakama hiyo kuzuia ugawaji mali za baba yake aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo, John Mwakipesile baada ya kutofika mahakamani hapo.

Mbali ya kuwa Mbunge wa Kyela, Mwakipesile pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Imeelezwa kuwa Septemba 5, Boniface chini ya wakili wake, Aikande Lema aliwasilisha shauri lake mwaka huu akipinga mali zilizogawiwa lakini pia akihitaji kurudiwa kikao cha familia ili kubainisha idadi ya mali, huku akipinga kuwa hana imani na msimamizi wa mirathi hiyo, Bupe Mwakipesile ambaye ni Mama yake wa kambo.

Akizungumza mahakamani hapo jana Jumatatu Oktoba 31, Hakimu mfawidhi mkazi wa mahakama hiyo, Andrew Njau amesema kutokana na mleta mashtaka kutotokea bila taarifa wala muwakilishi yeyote, ametupilia mbali ombi hilo.

Ameelezea kuwa katika kukuza, kuthamini na kuheshimu mahakama, hawawezi kuendelea na shauri hilo kwani hatua hiyo ni kama kuchezea mhimili huo.

"Waleta maombi waliiomba mahakama kuchunguza uhalali wa na haki katika usimamizi wa mirathi lakini hawajatokea, hakuna taarifa zozote wala uwakilishi kutoka kwa wakili yeyote hata kuomba msaada popote.

“Hivyo hii ni kama kuchezea mahakama na kwa mantiki hiyo kwa kuzingatia kifungu namba 95 sura ya 33 naondoa shauri hilo," amesema Njau.

Awali wakili wa upande wa mdaiwa, Hashim Mzirai ameiambia mahakama kuwa kutokana na upande wa waleta shauri kutotokea bila sababu zozote ombi hilo lifutwe, lakini walipe gharama zilizotumika kwa mdaiwa.

Akijibu ombi hilo, Njau amesema suala la kulipa gharama halipi nafasi kwani itakuwa ni kuchochea tena mvutano kwani kesi hiyo ni ya kifamilia.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Sekela Mwakipesile ambaye ni mtoto wa marehemu, amesema anaishukuru mahakama kwa kutenda haki kwani waleta malalamiko tangu kuanza kwa kesi hiyo hawajawahi kutokea.

"Sisi tunashukuru kwa uamuzi huu ambao tunaona umetenda haki kwa sababu wale walileta malalamiko lakini hawajahi kuja, hatujui wanalenga nini," amesema Sekela.

Chanzo: mwanachidigital