Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yatupa ombi la mawakili utetezi kesi ya Sabaya

Sabaya 1 1 Mahakama yatupa ombi la mawakili utetezi kesi ya Sabaya

Tue, 3 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imetupilia mbali ombi dogo la mawakili wa upande wa utetezi kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) la kutaka maelezo yaliyoandikwa kituo cha polisi na shahidi wa sita wa Jamhuri, Bakari Msangi (38), kusomwa mahakamani kama sehemu ya kumrejeshea kumbukumbu shahidi huyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni msaidizi wake wa karibu Sylvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38).

Wakili wa Utetezi, Sylvester Kahunduka, aliwasilisha ombi hilo mahakamani, akidai kwamba shahidi huyo amekuwa akihojiwa mambo mengi na majibu yake yamekuwa hakumbuki au hafahamu.

Alitumia kifungu cha Sheria ya Ushahidi Namba 168 (1,2), kuiomba mahakama hiyo kumsomea maelezo ya awali ya shahidi aliyoandika polisi ili kumrejeshea kumbukumbu.

Naye Fridolin Gwemelo Wakili wa Utetezi pia, aliiomba mahakama apatiwe maelezo ya shahidi ya polisi ili ayatumie kutikisa ushahidi wa shahidi.

Shahidi huyo alipewa kielelezo hicho cha nyaraka kuangalia kama anazifahamu na shahidi huyo, alithibitisha kuwa sahihi zilikuwa ni za kwake, lakini alidai kurasa za nyaraka hizo zilikuwa pungufu tofauti na alivyoandika maelezo awali.

Aidha, wakili huyo alidai kuwa pingamizi lililowekwa na Jamhuri la kutaka shahidi kufahamu kama alihojiwa kuhusu kufahamu maelezo yaliyoandikwa kituo cha polisi halikufuata takwa la kisheria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdalah Chavula, alidai kifungu cha sheria ya ushahidi 154 kimeelekeza nini kifanyike kwa kuwa maelezo yanatakiwa yawe yaliondikwa na kuzungumzwa na shahidi na kuwekwa kwenye maandishi.

Alidai kwamba maelezo ya polisi yaliandikishwa bila shahidi kupewa fursa ya kuyapitia na alitakiwa kusaini nyaraka hizo pasipo kufahamu kile kilichoandikwa na askari polisi.

Wakili Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka, alipinga ombi hilo.

“Utaratibu wa kisheria shahidi lazima atambue maelezo yake aliyoandika kwa utaratibu walipaswa kukumbuka kwa kurejea na maelezo yake aliyoandika kwa kusomewa, kuyaona na kuyatambua.”

“Mheshimiwa hakimu ukiangalia upande wa pili wanataka kutumia kifungu hiki cha sheria ya ushahidi kama kumrejeshea kumbukumbu shahidi kwenye maelezo yake ya awali aliyoandika kituo cha polisi, ilhali shahidi huyu, hajaomba kusomewa maelezo hayo kwa ajili ya kurejeshewa kumbukumbu,” alidai.

Naye Baraka Mgaya, Wakili wa Serikali, aliiomba mahakama hiyo, kumwelekeza wakili wa utetezi kuendelea kumhoji shahidi, badala ya kutumia mlango wa nyuma wa kisheria kutaka shahidi asomewe nyaraka ya polisi ili kumrejeshea kumbukumbu.

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Odira Amworo, akitoa uamuzi huo mdogo, alisema kifungu cha Sheria ya ushahidi namba 168(1,2), kinapaswa kutumiwa na upande ambao umepeleka shahidi mahakamani na kutupilia mbali ombi la mawakili wa utetezi.

Shahidi huyo, ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini, jijini Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amelitoa ushahidi kwa siku tano mfululizo.

Kesi hiyo imenguruma kwa siku 15 mfululizo katika mahakama hiyo.

Katika hatua nyingine, wakili wa upande wa utetezi, Fridolin Gwemelo, aliwasilisha ombi lingine mahakamani kuomba kutambua maelezo yaliyoandikwa kituo cha polisi kwa kuwa yanatofautiana na ushahidi wake alioutoa mahakamani.

“Hoja yangu huu sio wakati wa kuweka pingamizi au kuonyesha maelezo yamechukuliwa kihalali au hayakuchujwa kihalali bali huu ni wakati wa kumhoji shahidi,” alidai.

Akijibu hoja za utetezi, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, alidai kifungu cha Sheria ya ushahidi 154 kimeelekeza nini kifanyike kwa kuwa maelezo yanatakiwa yawe yaliondikwa na kuzungumza na shahidi na kuwekwa kwenye maandishi.

“Siyo sahihi kusema wanampitisha shahidi kwenye ushahidi wake wakati alishasema hana ufahamu kwa kile kilichoandikwa ilhali wanatambua na kuelewa kuwa shahidi hafahamu maelezo yaliyoandikwa mbali na kuona sahihi zake na kwa msimamo huu wa sheria vigezo vilivyoainishwa na kifungu cha sheria ya ushahidi namba 154 haiendani na kile kilichotokea.”

“Eti wakili anasema tumeweka pingamizi wakati ambao siyo wake na alikuwa anaendelea kujenga hoja, hii sio sahihi kabisa kwa kuwa alianza kwa kumuonyesha shahidi nyaraka ya maelezo kama saini ni za kwake na alikubali, lakini aliieleza mahakama kwamba hafahamu kilichoandikwa ndani kwenye maelezo kwa kuwa hajapata fursa ya kusomewa.

“Si kweli kwamba ni sahihi shahidi akitia saini maelezo yake ikawa ni ya kweli, inawezeka alitia saini lakini maelezo yakawa siyo sawa na sheria haisemi hivyo, pia maswali ambayo alikuwa akiulizwa shahidi yalikuwa yanaendana na maelezo yaliyotolewa polisi.”

Chanzo: ippmedia.com