Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yatilia shaka taarifa za ugonjwa wa mshtakiwa

Mahakama yatilia shaka taarifa za ugonjwa wa mshtakiwa

Fri, 6 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kufuatilia taarifa za ugonjwa wa mshtakiwa, George Ntalima kwa ofisa wa Magereza ili kujua hali yake.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo leo Alhamisi Desemba 5, 2019   baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani kwa mara ya pili mfululizo.

Ntalima ambaye ni ofisa usafirishaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na wenzake wanne  wanakabiliwa na mashtaka 55 yakiwemo ya kutakatisha fedha na  kuisababishia Serikali hasara ya  Sh1.175 bilioni.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Ladslaus Komanya ameieleza  mahakama hiyo leo kuwa, Ntalima ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo haonekani mahakamani.

Komanya ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Komanya amedai mshtakiwa Ntalima hayupo mahakamani, kumtaka wakili wa mshtakiwa kuieleza mahakama alipo mteja wake.

Komanya baada ya kueleza hayo, wakili wa mshtakiwa, Tully Kaundime amedai mteja wake ni mgonjwa anasumbuliwa na majipu yaliyosababisha homa kali na ndio sababu ya kushindwa kufika mahakamani.

Kaundime amedai afya ya mshtakiwa imezorota na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili Komanya amedai wakili wa mshtakiwa anatakiwa kutoa taarifa huku ikiambatanisha na taarifa rasmi kutoka Magereza  ili ijulikane kama anapatiwa matibabu au amepumzishwa.

"Ili kutenda haki kwa washtakiwa wengine wakili huyu anatakiwa alete uthibitisho kuhusu ugonjwa unaomsumbua mshtakiwa na sababu za kutompeleka mahakamani,” amedai Komanya.

Akijibu hoja ya upande wa mashtaka, Kaundime amedai mteja wake yupo mahabusu chini ya uangalizi wa Magereza, si sahihi kupeleka taarifa za ugonjwa au kueleza alipo mshtakiwa wakati wanafahamu yupo kwenye mikono salama ya Magereza.

Kaundime amedai wanaopaswa kutoa taarifa hiyo ni Magereza.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ally amesema ni wajibu wa upande wa mashtaka kupata taarifa za mshtakiwa huyo kutoka Magereza.

Ameutaka upande wa mashtaka kuwasiliana na Magereza kupata taarifa za mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama maendeleo yake.

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19, 2019 kwa ajili ya kuwasomea  maelezo ya awali.

 

Mbali na Ntalima, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni aliyekuwa mkurugenzi wa Nida, Dickson Maimu; meneja biashara wa mamlaka hiyo, Avelin Momburi; Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo na mkurugenzi wa sheria Nida, Sabina Raymond.

Kati ya mashtaka mapya 55 waliyosomewa washtakiwa hao, yapo ya  kuisababishia Serikali  hasara ya Sh1.175 bilioni, utakatishaji fedha, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri wao,  kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, matumizi mabaya ya madaraka na kuongoza genge la uhalifu.

Maimu, Ntalima na Silverius wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana. Momburi na Raymond wapo nje kwa dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz