Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yataka upelelezi kukamilika kesi ya bosi wa zamani Takukuru

56496 TAKUKURU+PIC

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji na Tathmini wa Takukuru, Kulthum Mansoor, kufuatilia  kujua upelelezi umefikia hatua gani.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka manane likiwamo la utakatishaji wa fedha Sh1.47 bilioni.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Takukuru, Pendo Temu, kuieleza Mahakama kuwa upelelezi haujakamilika.

Leo Alhamisi Mei 9, 2019 Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina amesema upande wa mashtaka uhakikishe unafuatilia ili kujua huo upelelezi umefikia kwenye hatua gani ili shauri hilo liendelee.

Baada ya maelezo hayo aliahirisha shauri hilo hadi Mei 23, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa ndani.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa alighushi tarehe tofauti Januari 2013 na Mei 2018 akiwa makao makuu ya Takukuru iliyopo jijini Dar es Salaam alitoa barua ya ofa ikionyesha barua hiyo imetoka katika Halmashauri ya Bagamoyo huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kosa lingine  tarehe tofauti kati ya Januari 2012 na Mei 2017 akiwa eneo la Upanga mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh 5.2 milioni kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Alex Mavika kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.

Katika kosa la utakatishaji wa fedha kati ya tarehe tofauti Januari mwaka 2013 na Mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh1.47 bilioni huku akijua fedha hizo ni zao la makosa mengine.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz