Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yataka upelelezi kesi ya kina Dk Tenga ukamilike

32787 Pic+tenga Tanzania Web Photo

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha upelelezi kwa wakati katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili Dk Ringo Tenga.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 21, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi ipo mahakamani hapo kwa muda mrefu hivyo upande wa mashtaka wahakikishe upelelezi unakamilika kwa wakati.

"Hii kesi imechukua muda mrefu sana hivyo upande wa mashtaka mnatakiwa kuhimiza ili upelelezi ukamilike hakuna mtu mwingine wa kulikwamua hili, sisi kazi yetu kuhakikisha majalada yanakwisha," amesema Hakimu Simba.

Hakimu Simba ameeleza hayo baada ya Wakili wa Serikali, Wankyo Simon kudai kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na kampuni ya Six Telecoms.

Baada yakueleza hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 4, 2019 kesi hiyo itakapotajwa.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadai kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao, wanadaiwa kwa kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Vile vile, washitakiwa hao wanadaiwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (zaidi ya Sh.8bilioni ).



Chanzo: mwananchi.co.tz