Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yataka uchunguzi kesi ya Tito wa LHRC kukamilika

Mahakama yataka uchunguzi kesi ya Tito wa LHRC kukamilika

Thu, 16 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu nchini Tanzania imeueleza  upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Tito Magoti  na mwenzake, Theodory Giyani kukamilisha upelelezi katika maeneo yaliyobaki ili kesi iendelee katika hatua nyingine.

Magoti ni ofisa programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Giyani ni mtaalamu wa Tehama wa kituo hicho. Wawili hao wanakabiliwa  na mashtaka matatu likiwemo la utakatishaji wa  Sh17 milioni.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Aprili 15, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo,  Janeth Mtega wakati shauri hilo lilipowasilishwa kwa ajili ya kutajwa.

 “Baada ya kupitia hoja za pande zote mahakama hii inaelekeza upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi katika maeneo yaliyobakia ili kesi hii iweze kuendelea na hatua nyingine” amesema Hakimu Mtega.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Faraji Nguka, amedai upelelezi haujamamilika na wameshafanya mawasiliano na wapelelezi wa kesi hiyo ili kukamilisha maeneo yaliyobaki kama walivyoelekezwa na mahakama hiyo wiki mbili zilizopita.

“Wapelelezi wetu wameahidi kukamilisha uchunguzi katika maeneo yalikuwa yamebakia kama ambavyo mahakama hii ilivyotuelekeza kufanya  hivyo   tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Simon.

Pia Soma

Advertisement
Upande wa mashtaka baada ya kueleza hayo wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha kesi hiyo kama mahakama ilivyoelekeza.

“Ni rai yetu upande wa mashtaka watakamilisha upelelezi kwa wakati kama walivyoelekezwa na mahakama kwa sababu mashtaka waliowashtaki nao wateja wetu hayana dhamana, hivyo walitakiwa kukamilisha upelelezi ndio wawashtaki,” amedai Mtobesya.

Akijibu hoja hiyo wakili Simon amedai kuwa wameipokea hoja iliyowasilishwa na upande wa utetezi na wataifanyia kazi.

Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi  Aprili 29, 2020 itakapotajwa tena huku washtakiwa wakirudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza wawili hao walifikishwa Kisutu Desemba 24, 2019 wakikabiliwa na mashtaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 137/2019.

Chanzo: mwananchi.co.tz