Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imesema kesi inayomkabili Ramadhan Mlaku ambaye ni Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) itakapokuja tena mahakamani hapo upande wa mashtaka wawe na majibu ya kutosha kwa kuwa shauri hilo lipo zaidi ya mwaka mmoja na upelelezi bado haujakamilika.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Candid Nasua kudai leo Jumanne Septemba 24, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa jalada halisi lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kupitiwa na kutolewa uamuzi.
Simba amesema tarehe ijayo shauri hilo lisipokuja mahakamani hapo upande wa mashtaka waeleze upelelezi umefikia kwenye hatua gani.
"Upelelezi umechukua muda mrefu hadi sasa ni mwaka mmoja na nusu, siyo rahisi kuahirisha bila ya kuwa na maelezo ya kutosha, nakuagiza ukawaambie nataka majibu shauri hilo litakapokuja tena," amesema Simba.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 8, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Kwa Mara ya kwanza shauri hili lilifikishwa mahakamani hapo Machi 14, 2018 ambapo mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la mauaji.
Pia Soma
- Boris ashangazwa wakurugenzi Thomas Cook kulipwa mamilioni
- DC Dodoma atangaza operesheni kuwasaka vibaka
- Simba, Nyati wapagawisha washiriki tamasha la Jamafest
- Tanzania kupewa uenyeji Jamafest 2032