Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yataka maelezo ya mashahidi kesi ya akina Dk Tenga

42000 Pic+tenga Mahakama yataka maelezo ya mashahidi kesi ya akina Dk Tenga

Sat, 16 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili vigogo wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili Dk Ringo Tenga, kesi hiyo itakapotajwa tena kuwa na majibu sahihi ya maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo.

Hayo yameelezwa na Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali,Ester Martine kudai mahakamani hapo kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi uko kwenye hatua za mwisho.

Hakimu Simba alisema shauri hilo litakapokuja mahakamani hapo upande wa mashtaka waje na majibu yaliyokamilika ya maelezo ya mashahidi.

Wakili wa Serikali Ester alidai kuwa wapo kwenye hatua za mwisho wa kukamilisha upelelezi na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa ili kama wapo tayari kufungua kesi Mahakama Kuu watatoa taarifa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi Mosi, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Mhandisi Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni wa hiyo, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadaiwa kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao, wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni,Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola  3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

 

Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola 3,748,751.22 (sawa na Sh. 8bilioni ).

 



Chanzo: mwananchi.co.tz