Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yataka kujua upelelezi wa vigogo wa madini ulipofikia

Tue, 6 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kulifuatilia jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi wa Serikali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Novemba 17, 2018 ueleze maendeleo halisi ya upelelezi wa kesi hiyo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ameeleza hayo leo Jumatatu Novemba 5, 2018 wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Ni baada ya Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde kuieleza Mahakama hiyo kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na kwamba DPP ametoa maelekezo ambayo yanafanyiwa Kazi.

Hivyo ameiomba kesi ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa, baada ya Wakili Mkunde kueleza hayo, Wakili wa utetezi Nehemiah Nkoko ameeleza inaumiza ni mwaka umepita shtaka moja upelelezi wake bado haujakamilika.

Nkoko amedai dhamana za washtakiwa DPP amezuia na kuhoji kuna makesi yenye mashtaka mengi upelelezi wake umekamilika ndani ya miezi mitatu, hili shtaka moja linatimiza mwaka mmoja  unaenda wa pili sasa.

Amedai katika shtaka linalowakabili washtakiwa hao, Nkoko amedai limejitosheleza na lina kila  kitu toka mwaka jana lugha ni upelelezi haujakamilika.

"Sisi tunaamini unapozuia dhamana ya mtu basi hiyo mtu atasikilizwa kwa wakati, tunaomba Mahakama iwalazimishe upande wa mashtaka wake na msimamo halisi wa upelelezi ili tujue wamekwama wapi na sisi tufuatilie,” amesema Nkoko.

Wakili Mkunde baada ya kusikiliza hoja za Wakili Nkoko, amedai uwepo wa shtaka moja katika kesi hiyo haina maana kuwa upelelezi wake utakuwa rahisi.

 

 

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Mashauri ameutaka upande wa mashtaka kulifuatilia jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi wa serikali kwa DPP na Novemba 17, 2018 ueleze maendeleo halisi ya upelelezi wa kesi hiyo.

Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania  (Tansort) Archard Kalugendo na mthamini almasi wa serikali, Edward Rweyemamu ambao ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini, wote walikuwepo mahakamani.

Kalugendo na Rweyemamu wanasota mahabusu kutokana na DPP kuzuia dhamana zao na wanakabiliwa na  kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh 2.4 bilioni.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia serikali hasara ya Sh2,486,397,982.54 ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017  katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

Washtakiwa hao wanadaiwa kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa almasi wa serikali na waajiriwa wa wizara hiyo waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 1,118,291.43  ambazo ni sawa na Sh2,486,397,9.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo ya Kisutu  haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Chanzo: mwananchi.co.tz