Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yasikiliza CD kesi ya Lukuvi

29496 Pic+makama TanzaniaWeb

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, imesikiliza sauti ya mazungumzo yaliyorekodiwa na kifaa maalumu cha kunasia sauti, kilichowekwa katika ofisi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Sauti hiyo ya dakika 30 iliyohifadhiwa katika CD, ilitolewa jana mahakamani hapo na mchunguzi wa Takukuru, Amar Ally (29) akitoa ushahidi katika kesi ya kutoa rushwa inayomkabili mfanyabiashara Mohamed Kiluwa.

Kwenye CD hiyo inasikika maongezi yanayodaiwa ni baina ya Lukuvi, Kiluwa na Kassim Ephraim ambaye ni mchunguzi kutoka Takukuru, ilitolewa mahakamani hapo kama kielelezo namba sita katika kesi hiyo.

Katika CD hiyo, Kiluwa anadaiwa kusikika akilia kwa sauti huku akitoa maneno ya kumtaka Lukuvi amsaidie baada ya kuambiwa yupo chini ya ulinzi na maofisa wa Takukuru.

Ally ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo, aliieleza Mahakama mbele ya Hakimu Samwel Obasi kuwa ndiye aliyehusika kupakua sauti iliyokuwa imerekodiwa kupitia kifaa maalumu.

Akiongozwa na wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo, shahidi huyo alidai Juni 16 aliletewa kifaa cha kielektroniki cha kunasia sauti kutoka kwa Ephraim kwa ajili ya kupakua (download) sauti hiyo na kuiweka katika CD.

Shahidi huyo ambaye yupo kitengo cha uchunguzi wa maabara ya kielektroniki inayohusu vifaa vya kielektroniki Takukuru makao makuu, alidai baada kupakua sauti hiyo Julai 19 alimrudishia Ephraim kifaa chake na kusaini fomu maalumu.

“Katika maabara yetu ya uchunguzi wa kielektroniki, tunafanya uchunguzi kwa vifaa vya kielektroniki vinavyoletwa kwetu, ambavyo ni simu, kinasa sauti (Tape Recorder), Flash, Disk na CD,’’ alidai.

Baada ya kupakua sauti hiyo alidai aliisikiliza kujua kama iliyopo katika tape recorder ndiyo hiyohiyo aliyoweka katika CD.

Alibainisha sababu ya kurekodi na kuthibitisha mambo yanayodaiwa kuzungumzwa baina ya Kiluwa na Lukuvi.

Katika CD hiyo iliyochezeshwa mahakamani hapo kwa kutumia kompyuta ya shahidi huyo, inasikika sauti inayodaiwa ya Kiluwa ikimpongeza Lukuvi kwa utendaji wake na kueleza kuwa hatamuangusha katika kutekeleza maagizo aliyopewa ya kuendeleza viwanja hivyo.

Pia. sauti hiyo inasikika ikimweleza Lukuvi kuwa alipigiwa simu na Steven Nyerere akimweleza kuwa viwanja anavyomiliki vina tatizo.

Katika sauti hiyo inasikika ikieleza kuwa amebeba Dola 40,000 za Marekani (zaidi ya Sh90 milioni) kama hela ya mafuta.

“Wewe ni kama ndugu yangu, ukiona nafanya vibaya niite nionye, nakupa hela hii ya mafuta kama ndugu,” inasikika sauti hiyo.

Hata hivyo, Lukuvi anasikika akimwambia: “Kama ni mafuta Serikali inatoa, vipi kwanza hati zangu za viwanja ziko wapi? Maana nilikwambia uje nazo leo.”

Sauti inayodaiwa kuwa ya mshtakiwa inajibu: “Hati za viwanja anazo mwekezaji mwenzangu ambaye yupo nchini Urusi, lakini majarida ya mpango mkakati ninayo hapa.”

Lukuvi: “Umeshawapa watu wangapi ambao wamekusaidia, ambao watu hao pia ndiyo walionitambulisha kwako? Baada ya kuulizwa hivyo, inasikika sauti ya inayodaiwa ya mshtakiwa akilia na kuomba Lukuvi amsaidie: “Naomba unisaidie kaka, kaka naomba unisaidie... brother (kaka) naomba unisaidie.”

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, mahakama iliahirishwa kwa muda hadi saa 8:30 mchana.

Wakili augua ghafla

Hata hivyo, Mahakama ilivyotokaa muda huo, kabla ya shahidi wa nne hajaanza kutoa ushahidi wake, wakili wa Kiluwa, Iman Madega alidai hali yake ya afya siyo nzuri hivyo anaomba kesi hiyo iahirishwe.

“Afya yangu haiko vizuri, ukilinganisha na asubuhi nilivyokuwa, hivyo naomba Mahakama iahirishe shauri hili hadi siku nyingine itakapopangwa,” aliomba Madega.

Baada ya maelezo hayo, hakimu Obasi aliahirisha kesi hadi Desemba 10 na 11 itakapoendelea, mshtakiwa yupo nje kwa dhamana



Chanzo: mwananchi.co.tz