Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yashindwa kulipa stahiki za mashahidi, kesi ya Gugai yakwama

61152 Pic+gugai

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara  nyingine imeshindwa kuendelea na usikilizwaji  wa ushahidi katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato halali, inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na mwenzake, kutokana mashahidi kushindwa kulipwa stahiki zao na uongozi wa Mahakama hiyo.

Mashahidi hao ambao wanatoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam, wameshindwa kuletwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kutokana na uongozi wa Mahakama ya Kisutu, kushindwa kuwalipa fedha zao, ambazo ni za usafiri na malazi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa ameeleza hayo leo Jumatatu, Juni 3, 2019 mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Mbagwa amedai wameshindwa kuwaleta mashahidi wengine  mahakamani hapo kutokana na mashahidi watano ambao walishatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao, kushindwa kulipwa fedha zao na uongozi wa Mahakama hiyo.

Amedai kwa kawaida mashahidi hulipwa baada ya kuja kutoa ushahidi mahakamani.

"Mheshimwa Hakimu, tumeshindwa kuleta mashahidi wetu kutoka mikoani kwa sababu, kuanzia shahidi wa tisa hadi 13 ambao tayari walishatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hawa, bado hawajalipwa stahiki zao hadi sasa," amedai Mbagwa

Pia Soma

"Tumefuatilia na kufanya jitihada za kutosha kuhusu suala hili, lakini bado uongozi wa mahakama umeendelea kutoa ahadi kuwa wanalifanyia kazi mpaka sasa, hivyo basi kutokana na mazingira hayo, tumeshindwa kuita mashahidi wengine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi,"  amedai Mbagwa.

Amedai mshahidi hao watano, ambao ni shahidi wa tisa  hadi 13 hawajalipwa stahiki zao kuanzia Machi 6, 2019 walipotoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao hadi sasa.

Amedai kutokana na hali hiyo wanaiomba mahakama itoe amri muhimu ili kuruhusu uongozi wa Mahakama hiyo, uweze kuwalipa stahiki zao mashahidi hao .

Mbagwa baada ya kueleza hayo, hakimu Simba amesema suala hilo linatatulika hivyo atalifuatilia.

"Suala hili linatatulika na mimi nitalifuatilia suala hili, ili kesi hii iweze kuendelea kwa sababu ni kesi ya muda mrefu, hivyo ninaipanga kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Juni 18, 20 na 24, 2019 itakapoendelea na ushahidi," amesema Hakimu Simba.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 17, 2019 itakapotajwa na kuanzia Juni 18, 20 na 24, mwaka 2019 kesi hiyo itaendelea na ushahidi.

Hii ni mara ya tatu kwa uongozi wa mahakama hiyo, kushindwa kutoa fedha kwa wakati kwa ajili ya kuwalipa  mashahidi wanaotoka nje ya mkoa wa Dar es  Salaam, kwani Oktoba 3, 2018, na Machi 26, 2019, kesi hiyo ilishindwa kuendelea na ushahidi kutoka na sababu hizo.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Tayari shahidi 13 wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 43; makosa 19 kati ya hayo  ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa, huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: mwananchi.co.tz