Moshi. Mahakama ya Hakimu mkazi mjini Moshi leo Juni 29, 2018 imeshindwa kufunga ushahidi wa kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Shule ya Scolastica, Humphery Makundi (16) ili kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kutokana na mkanganyiko wa tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji ni mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo, mwalimu Labani Nabiswa na mlinzi wa shule hiyo, Hamisi Chacha.
Juni 27, 2018 Hakimu mkazi wa Mahakama ya Moshi, Julieth Mawole aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vitakavyotumika dhidi yao lakini hawakufikishwa mahakamani kutokana na Magereza kunakili kimakosa tarehe.
Kutokana na hali hiyo wakili wa Jamhuri, Agatha Pima ameiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi na kupangiwa tarehe nyingine.
“Kesi ipangiwe tarehe nyingine kwani kumetokea tatizo la tarehe, washtakiwa hawakuandikiwa tarehe ya leo, rumande iliandika tarehe nyingine. Sisi upande wa Jamhuri tunasisitiza tuko tayari,” amesema.
Wakili anayemtetea mshatakiwa namba mbili, Elikunda Kipoko amesema hajaridhishwa na taarifa hizo na kutaka aelezwe kisa cha washtakiwa hao kutofikishwa mahakamani.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mawole alihoji sababu za washtakiwa kutofikishwa mahakamani licha ya kuwa alipanga kesi hiyo kuendelea leo.
Hata hivyo, Mawole ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 6, 2018 siku ambayo washtakiwa watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vitakavyotumika dhidi yao kwa ajili ya kufunga ushahidi kwenda Mahakama Kuu.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa Novemba mwaka jana na mwili wake kutupwa mita 300 kutoka shuleni hapo na ukazikwa bila kutambuliwa, hadi ulipofukuliwa kwa amri ya Mahakama.