Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaridhia kunyongwa aliyeua, kuficha maiti kwenye begi

63075 Pic+kunyongwa

Mon, 17 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Juhudi za raia wa India, Vinoth Praveen aliyehukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji kutaka kujiokoa dhidi ya adhabu hiyo zimegonga mwamba baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa yake.

Praveen alihukumiwa adhabu hiyo na Jaji Dk Fauz Twaib, Juni 20, 2011 baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya rafiki yake, Abdubasit Abdallah na kisha kuiweka maiti kwenye begi na kwenda kuitelekeza kwenye maegesho ya jengo la JM Mall ikiwa ndani ya gari.

Alikata rufaa akipinga hukumu hiyo, lakini Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu walioisikiliza, Sivangilwa Mwangesi, Dk Gerald Ndika na Ignas Kitusi, imetupilia mbali.

Badala yake, imepigilia msumari mwisho hukumu ya Mahakama Kuu ikisema ni sahihi.

Katika rufaa yake pamoja na mambo mengine, Praveen alidai kuwa Jaji Twaib alikosea kumtia hatiani kwa kuzingatia ushahidi wa kimazingira tu, kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha hatia dhidi yake ya kuua kwa kusudia.

Mahakama katika hukumu yake ilikubaliana na hoja za wakili wa mrufani, Melkiori Sanga na kutupilia mbali taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo ya daktari na maelezo ya mshtakiwa ya kukiri kutenda kosa hilo alipohojiwa na Polisi kutokana na kasoro za kisheria.

Pia Soma

Hata hivyo, Mahakama ilisema mwenendo wa mrufani baada ya tukio unadhihirisha kuwa alikuwa amedhamiria kutekeleza mauaji hayo.

Mwenendo huo ni pamoja na kuiweka maiti ndani ya begi, kwenda kuitelekeza ndani ya gari katika maegesho ya hoteli na vitendo vyake kabla na baada ya tukio kama vile kumpeleka mkewe nyumbani kwao na kujaribu kutoroka baada ya tukio.

Praveen alimuua Abdubasit ambaye alikuwa Mtanzania mwenye asili ya India, Februari 6, 2009, alipomuita nyumbani kwake, Mtaa wa Kipata, Kariakoo, jijini Dar es Salaam kwa kumchomachoma sehemu mbalimbali za mwili akitumia visu viwili na mishale.

Kisha aliweka mwili huo ndani ya begi la nguo, akauweka kwenye gari na kwenda kulitelekeza gari hilo kwenye maegesho ya jengo la JM Mall.

Mwili huo uligunduliwa na walinzi wa jengo hilo Februari 8, siku mbili baadaye baada ya kuona gari hilo limekaa hapo muda wote huo bila mwenyewe kuonekana.

Walitoa taarifa kituo cha polisi ambao walifika eneo la tukio na kulifungua ndipo walipokuta mwili huo ndani ya begi kwenye kiti cha nyuma ukiwa umeshaanza kunuka.

Praveen alitiwa mbaroni na polisi akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akitaka kutoroka kwenda kwao India, huku akiwa na ufunguo wa gari ilimokuwa maiti hiyo.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi saba akiwamo mlinzi wa eneo la majengo alikokuwa akiishi mshtakiwa, ambaye alimshuhudia akiingia ndani akiwa na Abdubasit na baadaye akatoka peke yake akiwa na begi ambalo alimsaidia kuliingiza ndani ya gari bila kujua kilichokuwamo.

Pia uliwasilisha mahakamani vielelezo 23, likiwamo begi ambamo mwili huo ulikutwa, visu viwili na mishale vilivyotumika kutekeleza mauaji hayo.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo baada ya kukerwa na kitendo cha Abdubasit kumdai deni lake la Dola za Marekani 20,000 alizokuwa amemkopesha, miezi mitatu kinyume cha makubaliano ya kurejesha mkopo ndani ya mwaka mmoja.

Katika utetezi wake, mahakamani, ingawa alikiri kutenda kosa hilo, alikana kutenda kwa makusudi badala yake alidai kuwa alifanya hivyo wakati akijitetea baada ya Abdubasit kuanza kumshambulia kwa fimbo wakati wakijadili namna ya kulipa deni hilo.

Hata hivyo Jaji Twaib alitupilia mbali utetezi wake na akakubaliana na ushahidi wa upande wa mashtaka, hivyo kumtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz