Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaridhia kikao mgogoro KKKT Konde

Konde Mahakama yatoa neno mgogoro KKKT Konde

Thu, 19 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu kanda ya Mbeya imeridhia ombi la kufanyika kwa kikao cha usuluhishi nje ya Mahakama ya kati ya upande wa aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania KKKT, Dayosisi ya Konde, Dk. Edward Mwaikali na Askofu Mteule, Mchungaji Geofrey Mwakibaha

Dk. Mwaikali ndiye aliwasilisha maombi ya kupinga uamuzi wa kuondolewa madarakani dhidi ya uongozi mpya chini ya Askofu Mteule Mwakihaba ambaye alichaguliwa kwenye mkutano mkuu uliofanyika Machi 22 mwaka huu na kusimamiwa na Mkuu wa Kanisa hilo nchini Askofu Dk. Fredrick Shoo.

Jaji  James Karayemaha alitangaza uamuzi huo, jana wakati wa kusikiliza shauri hilo ambalo lilihusisha waumini, viongozi wa Kanisa hilo na mawakili wa pande zote mbili.

Jaji Karayemaha alitoa baraka za kufanyika kwa maridhiano ya pamoja nje ya mahakama na kwamba njia hiyo ni nzuri kwani itawaleta pamoja viongozi wote hao na kujadili namna bora ya kumaliza mgogoro huo, ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

“Nimesikiliza hoja za pande mbili wa wajibu maombi na  wapeleka maombi, kimsingi hapa busara inapaswa kutumika ili kupata usuluhishi juu ya mgogoro huu licha ya kuwa kila upande una hoja zake lakini, jambo hili linahusu masuala ya imani na dini hivyo kufanyika kwa maridhiano kutaleta amani ndani ya mioyo ya waumini, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla,” alisema Jaji Karayemaha.

Alieleza mahakama kuwa miongoni mwa majukumu ya chombo hicho ni kushauri kufanyika maridhiano na usuluhishi kwenye mambo yanayohusu imani za kidini ili kutengeneza amani na utulivu na kuokoa gharama za muenendo wa kesi hiyo.

“Nina imani muda wa wiki moja ambao umetolewa kushughulikia mgogoro huu kwa kufanya vikao vya usuluhishi kati ya pande zote mbili ndani ya Dayosisi hiyo ya Konde, utasaidia kesi hii ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo kumalizika mapema ili watu wakaendelee na shughuli za maendeleo aliongeza,” alieleza Jaji Karayemaha.

Aidha Jaji Karayemaha alimpongeza  Dk. Mwaikali kupeleka mahakamani ombi la kufanyika kwa usuluhishi wa mgogoro huo nje ya mahakama kwa maelezo kuwa njia hiyo ni ya busara na inaonyesha imani na utulivu katika Kanisa hilo.

Alisema shauri la ombi la pingamizi kuondolewa madarakani  kwa Dk. Mwaikali limepangwa kusikilizwa tena Mei 31, mwaka huu  baada ya kikao cha usuluhishi kukaa.

Awali mahakamani hapo, Wakili upande wa mashtaka, Samson Mbamba aliieleza mahakama kuwa kuna mazungumzo ya usuluhishi kuhusu mgogoro huo yameanza yakihusisha viongozi wa pande zote mbili pamoja na vyombo vya serikali.

Aliiomba mahakama kuwa ni vyema shauri hilo likasimamishwa kwanza mahakamani ili kuruhusu vikao vya maridhiano vifanyike ndio hatua nyingine ziendelee.

Wakili upande wa utetezi, Dk. Daniel Pallangyo alieleza kuridhia kufanyika kwa vikao vya usuluhishi ili kumaliza mgogoro huo licha ya hapo awali kuomba shauri hilo liendelee kwani hakukuwapo taarifa zozote juu ya kuanza kwa usluhishi.

Baada ya mahakama hiyo kutoa ridhaa ya kufanyika Dk. Mwaikali aliwaomba viongozi wa kanisa hilo waumini na watu wengine kudumisha amani na utulivu wakati suala hilo likiendelea kufanyiwa kazi.

Mgogoro  huo ulianza kufukuta baada ya kuhamishwa kwa Makao Makuu ya Dayosisi hiyo kutoka Tukuyu wilayani Rungwe kwenda jijini Mbeya na kusababisha pande mbili kuanza kusigana.

 

Chanzo: www.tanzaniaweb.live