Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yapokea ramani mauaji ya trafiki aliyepigwa risasi kwenye mataa

RISASI 2222222222 Mahakama yapokea ramani mauaji ya trafiki aliyepigwa risasi kwenye mataa

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea ramani ya tukio la mauaji ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Sajenti Mensah aliyeuawa akiwa kazini eneo la mataa ya Sayansi, Kijitonyama Julai 22, 2016 kama kielelezo katika kesi hiyo.

Kijana Amani Filipo anatuhumiwa kumuua Sajenti Mensah kwa kumpiga risasi baada ya kumvamia katika kibanda cha polisi cha kupumzikia kilichoko mataa ya Sayansi kwa lengo la kutaka kupora.

Kielelezo hicho kilipokewa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya wa Mahakama hiyo baada ya shahidi namba tano, askari polisi Hassan Luto kuiomba Mahakama ikipokee kama kielelezo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Yasinta Lyimo, Luto ambaye ni mpelelezi wa kesi hiyo, alidai kuwa Julai 23, 2016, alikuwa kazini akiendelea na majukumu yake ya kazi.

Alidai kuwa aliitwa na mkubwa wa kazi yeye na wenzake wawili; Sajenti Bisima na Sajenti Ndege, wakipewa jalada la mauaji ya Sajenti Mensah kwa ajili ya upelelezi na walikwenda eneo la tukio.

"Tulikuwa tunalifahamu eneo hilo, lakini tulikuwa tukiongozwa na askari Ashirafu ambaye siku ya tukio alikuwapo, kwa hiyo alichora ramani ya tukio hilo na kuhoji mashahidi mbalimbali katika eneo hilo," alidai.

Luto alidai kuwa ramani hiyo aliyoichora ilionyesha Sajenti Mensah pamoja na shemeji yake wakati tukio linatokea walikuwa wamesimama, shemeji yake akiwa nje ya kibanda hicho.

"Ninaitambua ramani hii kwa sababu niliichora na nimeweza kuitambua kwa sababu ya mwandiko wangu na sahihi yangu, ninaiomba mahakama ipokee kama kielelezo katika kesi hii," aliomba Luto.

Hakimu Mbuya alikubaliana na ombi hilo, akapokea kielelezo hicho, ambapo upande wa mashtaka umefunga ushahidi wa mashahidi sita na mshtakiwa Amani ataanza kujitetea kesho.

Luto akijibu maswali ya Wakili wa mshtakiwa, Hassan Kiangio alidai eneo la Kijitonyama lina benki, lakini si benki zote zinalindwa na askari polisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live