Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaomba siku mbili kupitia jalada vigogo Rahco

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Machi 27, 2019 imeomba siku mbili kupitia jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco).

Vigogo wanaoshtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, Benhardard Tito, mwanasheria wa zamani wa kampuni hiyo, Emmanuel Massawe na mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma

Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo kuieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya uamuzi.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema jalada la kesi hiyo limeletwa asubuhi ya leo na ameanza kulipitia hivyo ndani ya siku mbili atakuwa amemaliza.

"Najua shauri hili ni la muda mrefu jalada la kesi hii nimeletewa asubuhi hii ndiyo nimeanza kulipitia hivyo ndani ya siku mbili nitakuwa nimemaliza,"alisema Simba.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 2, 2019 itakapokuja tena kwa ajili ya maamuzi.

Februari 27, 2019 wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya alitoa hoja na kudai kuwa kesi za uhujumu uchumi zinasikilizwa na Mahakama Kuu na alitaka upande wa utetezi kupewa nakala za nyaraka za mashahidi na vielelezo vyote.

Baada ya kutolewa hoja hiyo upande wa mashtaka uliieleza mahakama hiyo kuwa kwa mujibu wa sheria, inaelekeza kupewa maelezo ya mlalamikaji tu ikiwa atatumika kama shahidi katika kesi husika.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa walikula njama kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Ilidaiwa kuwa Februari 27, 2015 katika ofisi za Rahco, Ilala, Tito alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahco.

Ilidaiwa kuwa Tito na Massawe, Machi 12, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala wakiwa katika nyadhifa zao, walisaini barua ya kuihalalisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi huo.

Katika shtaka jingine, ilidaiwa kuwa Tito na Massawe, Machi 12 na Mei 20, 2015 wilayani Ilala walishindwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini na Rahco.

Tito na Massawe wanadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi za Rahco, kwa kutumia madaraka yao vibaya walisaini mkataba wa kutoa huduma za ushauri na kampuni ya Afrika Kusini bila ridhaa ya Bodi ya Zabuni ya Rahco.

Washtakiwa hao, wanadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kuwasilisha mkataba walioingia na kampuni ya Afrika Kusini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tito, Mwinyijuma na Massawe, wanadaiwa kati ya Machi mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi za Rahco, waliipa kazi kampuni hiyo ya ushauri na kuilipa kwa kutoa huduma za ushauri, malipo ambayo yalisababisha Rahaco kupata hasara ya dola za Marekani 527,540.

Ilidaiwa kuwa Agosti 18, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala, Tito alitumia madaraka yake vibaya aliipa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China kazi ya kujenga kilomita mbili za reli maeneo ya Soga iliyogharimu Dola 2,312,229.39 bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahco.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz