Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yamuhukumu kifungo cha nje aliyeiba mtoto Musoma

3eb09e962357b56eb3d118b9658dfd64 Mahakama yamuhukumu kifungo cha nje aliyeiba mtoto Musoma

Wed, 30 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma mkoani Mara imemhukumu mtoto (jina linahifadhiwa) kifungo cha nje kwa miezi sita baada ya kukiri kuiba mtoto mwenye umri wa miaka mitatu na miezi sita (majina yanahifadhiwa), mkazi wa Mtaa wa Nyakato Mlimani katika Manispaa ya Musoma.

Hakimu wa mahakama hiyo, Stanley Mwakihaba alitoa hukumu hiyo baada ya kumtia hatiani mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 15.

Awali binti huyo alipandishwa kizimbani na Wakili wa Serikali, Monica Hokololo Machi 15 mwaka huu akiwa mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya jinai Namba 48 ya mwaka 2022 na mshitakiwa wa pili, Juliet Makoye (43).

Wakili Monica alieleza mahakamani kuwa kosa hilo lilitendwa Februari 10 mwaka huu, kinyume na Kifungu 169(1)(a) cha Kanuni za Adhabu Na.16 na mapitio yake ya Mwaka 2019. Mtoto huyo alikiri kutenda kosa hilo, mshitakiwa wa pili alikana lakini alikiri kumfahamu binti huyo kwamba ni mama yake mkubwa na amemlea tangu akiwa mchanga baada ya kufiwa na mama yake mzazi.

Hokololo alieleza mahakama kuwa mtoto aliyenusurika kuibwa alikuwa ameketi nje nyumbani kwao, mshitakiwa wa kwanza alimuita na aliondoka naye hadi mbali kidogo, akamfumua nywele na kumbadili nguo kwa lengo la kubadilisha muonekano wake na kumbeba mgongoni akimfunika kwa kanga.

Mahakama ilielezwa kuwa baada ya kuzurura mitaani mpaka nyakati za usiku, walikutana na mwendesha pikipiki aliyehoji sababu za wao kuwa mitaani usiku huo na binti alieleza kuwa pamoja na mdogo wake (mtoto aliyemuiba) walitoka Geita wakimtafuta mama yao anayeishi Musoma.

“Mwendesha bodaboda ambaye majina yake hayakupatikana mara moja aliwapeleka nyumbani kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigera A, Simon Maregesi naye aliwapeleka kituo cha polisi kati cha Musoma ambako baada ya mahojiano ilichukuliwa ni tukio la kawaida la watoto kupotea, waliombewa hifadhi kwenye kituo cha kulelela watoto cha Jipe Moyo,” alisema Hokololo.

Siku iliyofuata wazazi wa mtoto aliyeibwa walifika kwenye kituo hicho cha polisi wakieleza upotevu wa mtoto wao na walipokutanishwa na watoto waliohifadhiwa kwenye kituo cha Jipe Moyo, ilibainika kuwa mtoto mdogo kati ya wale wawili ndiye aliyekuwa akitafutwa na wazazi hao.

Polisi ilianza upelelezi na binti huyo alikiri kuwa awali alidanganya kwani hakuwa dada wa mtoto husika bali alimuiba baada ya kumkuta amekaa nyumbani kwao, lengo likiwa kumpeleka Geita kwa ajili ya shughuli za kishirikina.

Binti huyo alisema amekuwa akiiba watoto wenye umri kati ya miaka miwili mpaka mitano kwa maelekezo ya mama yake (Julieth) na kwamba alishafanya wizi huo maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo Mwanza, Geita, Katoro huku Mara ikiwa mara yake ya kwanza.

Mtoto huyo alieleza polisi kuwa watoto hao wanapofikishwa Geita huchinjwa, baadhi ya viungo huuzwa na Julieth kwa wachimbaji wadogo wa madini na nyama wakizitumia kama kitoweo nyumbani na kwenye mgahawa wa Julieth.

Polisi walifuatilia na kumkamata Julieth akiwa mgahawani kwake Geita, alipandishwa kizimbani Machi 15 mwaka huu, alikana kutenda makosa hayo na pia jana alikana.

Jana alidhaminiwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh 2,000,000 kila mmoja. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 21 mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live