Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yamruhusu mhasibu kufungua tena kesi kumpinga Rais

HUKUMU Mahakama yamruhusu mhasibu kufungua tena kesi kumpinga Rais

Thu, 4 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Masjala Kuu imempa siku 14, aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Pere Muganda kufungua tena shauri la maombi ya mapitio kupinga uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia kufukuzwa kwake kazi.

Uamuzi huo umetolewa jana Jumatano Aprili 3, 2024 na Jaji Athuman Matuma, baada ya kukubaliana na maombi ya Muganda, kuongezewa muda kufungua shauri hilo, baada ya shauri alilolifungua awali kutupiliwa mbali na Mahakama hiyo.

Katika uamuzi huo, Jaji Matuma amesema amezingatia Muganda aliomba ridhaa ya Mahakama kufungua shauri hilo la mapitio ya Mahakama mapema ndani ya muda baada ya kumaliza hatua zote za kutafuta nafuu anazozitafuta.

Pia Jaji Matuma amesema hata baada ya kupata ridhaa hiyo alifungua shauri hilo la mapitio ya Mahakama mara moja bila kuchelewa.

“Ninaona hakuna madhara kwa wajibu maombi ikiwa maombi haya yatakubaliwa, zaidi ninaona ni mwombaji ndiye atakayeathirika kwa kunyimwa fursa kujaribu kupambania ajira yake wakati amekwishaonyesha uangalifu na juhudi za kuipambania,” amesema Jaji Matuma kwa tafsiri isiyo rasmi na kuongeza:

“Kwa hiyo ninakubali haya maombi na ninamuongezea mwombaji (Muganda) siku 14 kutoka tarehe ya uamuzi huu kufungua upya shauri hilo la mapitio ya mahakama. Hakuna amri kuhusu gharama.”

Muganda alikuwa ameajiriwa na Halmashauri ya Wilaya ya Siha katika nafasi ya uhasibu, lakini aliondolewa katika utumishi huo kwa madai sababu za kinidhamu.

Alijaribu kupinga uamuzi huo kwa njia za kiutawala bila mafanikio, baada ya kukata rufaa katika mamlaka zote za kiutumishi lakini rufaa zake zote zikatupiliwa.

Rufaa yake ya mwisho alikata kwa Rais ambaye ndiye mamlaka ya mwisho ya masuala ya utumishi wa umma, ambaye pia alitupilia mbali rufaa yake na kubariki uamuzi wa Tume ya Utumishi wa Umma iliyobariki uamuzi wa kufukuzwa kwake.

Hivyo, baada ya jitihada zake katika mamlaka za kiutawala kutokuzaa matunda ndipo alipokwenda mahakamani akaomba ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kupinga uamuzi huo wa Rais na akafanikiwa kupewa ridhaa hiyo baada ya kuiridhisha Mahakama kuwa alikuwa amekidhi vigezo.

Baada ya kupata ridhaa hiyo, Muganda alifungua shauri rasmi la mapitio ya Mahakama ndani ya muda uliowekwa kisheria kufungua mashauri kama hayo dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Halmashauri ya Wilaya ya Siha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hata hivyo, shauri hilo lilitupiliwa mbali Novemba 30, 2023 kutokana na sababu za kiufundi wa kisheria, baada ya kuwekewa pingamizi na wajibu maombi kwa hoja ambazo Mahakama ilikubaliana nazo.

Wakati shauri lake hilo linatupiliwa mbali, tarehe hiyo tayari alikuwa ameshakuwa nje ya muda kuweza kufungua tena shauri hilo baada ya kurekebisha kasoro za kisheria zilizobainika.

Hivyo alilazimika kwanza kufungua maombi ya kuongezewa muda kufungua shauri hilo la mapitio, chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Ukomo, lakini pia hakuweza kufungua maombi hayo mapema mpaka Desemba 23, 2023, siku 23 baadaye.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Muganda aliwakilishwa na wakili Isack Tasinga na wajibu maombi waliwakilishwa na mawakili wa Serikali--- Ayoub Sanga na Mathew Fuko.

Wakili Tasinga alilieleza Mahakama kuwa mteja wake alichelewa kwa muda huo kufungua maombi hayo kwa kuwa alichelewa kupata nakala ya uamuzi wa kutupilia mbali shauri lake la mapitio ya Mahakama.

Alidai aliata nakala ya uamuzi huo Desemba 19, 2023 kutoka katika tovuti ya Mahakama iitwayo Tanzlii, baada ya kuelekezwa hivyo na maofisa wa Mahakama na kwamba alifungua maombi hayo baada ya siku nne tangu tarehe aliyoipata.

Hivyo, aliiomba Mahakama hiyo iyakubali maombi hayo ya mteja wake kuongezewa muda akidai kuwa kukubaliwa kwa maombi hayo ya kuongezewa muda hayaathiri haki za wajibu maonmbi.

Kwa upande wake, Wakili Sanga alipinga hoja za upande wa mwombaji akidai hawakuwasilisha barua kuonyesha kuwa waliomba nakala ya uamuzi huo, wala mwombaji hakuwasilisha kiapo cha ofisa wa mahakama aliyekuwa anafuatilia kwake nakala hiyo.

Wakili Sanga alidai haikuwa muhimu nakala ya uamuzi wa kutupilia mbali shauri la awali kuambatanishwa na maombi ya kuongezewa muda kufungua tena shauri hilo, hivyo mwombaji hakupaswa kukaa muda wote huo wa siku 23.

Hata hivyo, Jaji Matuma baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake amekubaliana na hoja za mwombaji.

Jaji Matuma amesema nakala ya uamuzi wa shauri lililotupwa muhimu kuambatanishwa kwenye maombi hayo ya kuongezewa muda, ili kuthibitisha sababu za kuchelewa kwake.

Jaji Matuma amesema kuwa ingawa anakubaliana na wakili Sanga kuwa ushahidi wa nyaraka ni muhimu (kuhusu suala la barua ya Muganda kuomba nakala ya uamuzi mahakamani au kiapo cha afisa wa mahakama), lakini amesema kuwa si kila wakati ni muhimu.

Amefafanua kuwa inategemeana na kila aina ya kesi na kwamba katika shauri hilo uchelewaji ulikuwa ni siku 23 tu, ambazo kwa mtizamo wake ni muda mfupi ambao haukumlazimu mwombaji kutafuta ushahidi wa nyaraka.

Pia Jaji Matupa amesema mwombaji alieleza katika kiapo chake kwamba alikuwa anafuatilia nakala hiyo mahakamani kwa mdomo, utaratibu ambao pia unakubalika hasa kwa mwananchi wa kawaida na kwamba ingekuwa tofauti kama suala hilo lingekuwa limeshughulikiwa na mawakili ambao kawaida huwasiliana kwa maandishi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live