Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yamhukumu raia wa Uganda miaka mitatu jela au faini ya Sh1 milioni

29745 Mahakama+pic TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi.  Raia wa Uganda, Sureshbabu Kakolu, amehukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kutoa rushwa ya Dola 2,000 za Marekani, ambazo ni sawa na Sh4.5 milioni za Tanzania.

Kakolu ambaye ni meneja wa Fedha wa kampuni mbili za ujenzi amehukumiwa adhabu hiyo jana Ijumaa Novemba 30, 2018 na Hakimu Mkazi mwandamizi wa wilaya ya Moshi, baada ya kukiri kosa hilo ambalo awali Novemba 16, 2018 alilikana.

Kakolu alishitakiwa Novemba 15, 2018, alitoa fedha hizo kwa Meneja wa TRA mkoa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo ili apitishe maombi ya msamaha wa malimbikizo ya kodi yanayofikia Sh6.6 bilioni, ambazo kampuni hizo zinadaiwa na TRA.

Mshitakiwa huyo anashikilia wadhifa wa Meneja wa Fedha katika kampuni hizo mbili za ujenzi zinazotwa Dott Services (TZ) Ltd na General Nile Company for Roads and Bridges/Dott Services JV.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Holle Makungu, imesema raia huyo alikiri kosa hilo baada ya kusomewa kwa mara ya pili na mwendesha mashitaka wa taasisi hiyo, Rehema Mteta.

"Mshitakiwa amelipa faini aliyoamriwa na mahakama na fedha za rushwa alizotoa kwa Meneja wa TRA mkoa Kilimanjaro zitaingizwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali," ameeleza Makungu katika taarifa yake kwa wanahabari.

"Takukuru inatoa rai kwa watumishi wote wa umma na Taasisi za Serikali kutofumbia macho vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya raia wa kigeni," alisisitiza Makungu katika taarifa hiyo.

Akimsomea mashitaka yake, Mteta amedai Novemba 15, 2018 katika ofisi za TRA, mshitakiwa alitoa Dola 2000 za Marekani kwa meneja huyo, kama kishawishi ili apitishie maombi ya msamaha wa kodi.

Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo, hadi kufikia Oktoba 25, 2018, kampuni hizo mbili zilikuwa zikidaiwa kodi ya Sh6.6 bilioni ambayo ni malimbikizo ya kodi ya kati ya 2013 na 2018.

Baada ya kusomewa tena shitaka hilo hiyo leo Ijumaa, mshitakiwa amekiri kosa hilo ambapo upande wa mashitaka ukiongozwa na Mteta, ulimsomea maelezo ya kina ya kosa alilokiri mahakamani.

Katika maelezo hayo ya namna kosa lilivyotendeka, hadi kufikia Agosti 21,2018, makampuni hayo yalikuwa yakidaiwa malimbikizo ya kodi ya zaidi ya Sh5.7 bilioni, na kufikia Oktoba 25 likafikia Sh6.6 bilioni.

Katika kushughulikia madeni hayo na kupata msamaha wa kodi, alionana na meneja huyo wa TRA mkoa Kilimanjaro na kuahidi kutoa kiasi hicho ili amsaidie kufanikisha maombi yake hayo ya kusamehewa Sh6.6 bilioni za kodi.

Maofisa wa Takukuru waliandaa mtego na kufanikiwa kumkamata Kakolu papo hapo (red handed) wakati akitoa fedha hizo , ambalo ni kosa chini ya sheria za Takukuru.



Chanzo: mwananchi.co.tz