Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yakataa ombi la mmiliki shule ya Scolastica

10226 Shule+pic TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imekataa ombi la mmiliki wa Shule ya Scolastica, Edward Shayo anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo la kwenda kutibiwa.

Shayo, mwalimu wa shule hiyo, Labani Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha wanadaiwa kumuua mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo, Humphrey Makundi (16).

Ombi hilo liliwasilishwa jana na wakili Elikunda Kipoko anayemtetea mshtakiwa aliyeiomba mahakama itoe kibali akatibiwe ingawa hakusema mteja wake anaumwa nini.

Hakimu Mkazi Julieth Mawole alisema ingawa kutibiwa ni haki ya mshtakiwa, mahakama haina uwezo wa kutoa kibali hicho kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

“Mgonjwa ana haki ya msingi ya kupewa matibabu lakini mahakama hii haihusiki kutoa kibali, Magereza ndio inahusika kumpeleka mshtakiwa hospitali,” alisema.

Hakimu alisema, “Mimi sina mamlaka ya kumruhusu mshtakiwa kupelekwa hospitali, hiyo ni kazi ya Mahakama Kuu.”

Hayo yalijitokeza jana baada ya upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na wakili wa Serikali, Agatha Pima kuiarifu mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Baada ya kutolewa taarifa hiyo, Hakimu Mawole aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 29 washtakiwa watakaposomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vitakavyotumika dhidi yao.

Mwanafunzi Humphrey anadaiwa kuuawa Novemba mwaka jana na mwili wake kutupwa mita 300 kutoka eneo la shule hiyo na ukazikwa bila kutambuliwa hadi ulipofukuliwa kwa amri ya Mahakama.

Chanzo: mwananchi.co.tz