Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yakataa kubadili jina la Mwanyika

81754 Mahakama+pic

Sat, 26 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imekataa ombi la upande wa utetezi  kutaka kubadilisha  jina la Deogratius Mwanyika.

Mwanyika aliyekuwa rais wa mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Mshtakiwa huyo amewasilisha ombi hilo leo Ijumaa Oktoba 25, 2019 kupitia wakili wake, Flora Jacob akitaka jina lake la kwanza katika hati ya mashtaka lisomeke  Deodatus na si Deogratius.

Mwanyika na wenzake sita wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji fedha na kukwepa kodi katika kesi ya uhujumu uchumi namba 77/2018.

Wakili Jacob aliwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Amewasilisha ombi hilo muda mfupi baada ya wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Pia Soma

Advertisement
Jacob amedai kuwa jina la kwanza la Deogratius  katika hati ya mashtaka limekosewa hivyo anaomba upande wa mashtaka wafanye marekebisho.

Amedai mteja wake anaitwa Deodatus Mwanyika na si Deogratius Mwanyika kama inavyosomea katika hati ya mashtaka.

Wakati Jacob akiwasilisha ombi hilo,  Gasper Nyika ambaye ni wakili wa utetezi alitaka kujua upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua gani kwa sababu wateja wake wapo gerezani kwa muda wa mwaka mmoja sasa bila upelelezi kukamilika.

"Sio sahihi sisi upande wa utetezi kuhoji upelelezi wa kesi hii umefika hatua gani, na sio lazima kila siku upande wa utetezi tuhoji upelelezi umefikia hatua gani,” amesema Nyika.

Akijibu suala hilo Simon amedai hawezi kusema ni lini upelelezi wa kesi hiyo utakamilika na ataendelea kufuatilia kwa wapelelezi wa kesi hiyo kujua imefikia hatua gani.

Kuhusu kurekebisha jina la mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, amesema mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kubadilisha  chochote katika hati ya mashtaka.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alitoa uamuzi kwa kubainisha kuwa ili ibadilishe jina lazima iwe imesikiliza ushahidi.

"Jina haliwezi kubadilishwa wakati washtakiwa bado hawajasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo lakini kesi upelelezi wake bado haujakamilika, sasa tutajuaje kama jina lililopo katika hati ya mashtaka limekosewa,” amesema Hakimu Mhina.

Hakimu Mhina baada ya kueleza hayo aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, 2019.

Mbali na Mwanyika, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja uhusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo;  Mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku, Assa Mwaipopo; kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration Du Nord LTEE na Bulyanhulu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya Dola  112 milioni.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, saba ya kughushi, 17 ya utakatishaji fedha, kuwasilisha nyaraka  za uongo kwa TRA shtaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka nane ya kukwepa kodi na moja la kutoa rushwa.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30,2007 katika sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera, maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maeneo mengine ambayo washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo ni katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na Uingereza.

Aidha washtakiwa Mwanyika  na Lugendo wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa kamishna jenerali wa TRA huko Biharamulo kwa nia ya kukwepa kodi ya Dola 9.3 milioni ambayo ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha fedha Dola 374,243,943.45  za Marekani huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

Pia,  washtakiwa wanadaiwa kati ya Novemba 2,  2012 na Novemba 27, 2015 huko Shinyanga walitoa rushwa ya Sh718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye  ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kughushi washtakiwa hao wakiwa na nia ya ulaghai walighushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30, 2014 Kampuni ya Pangea Limited ilikubali kukopa Dola 90,000,000 ikiwa na riba Kutoka Benki ya Kimataifa ya Barrick huku wakijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la kutoa nyaraka ya uongo, mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30, 2018 huko BOT wilaya ya Ilala, kwa makusudi aliwasilisha nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya kampuni mgodi wa Bulyanhulu na Barrick International Bank Corp kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, kati ya Juni 2001 na Desemba 13, 2007 Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa Dola 416,100,000 kutoka Barrick.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz