Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaiamuru Tanzania kufuta adhabu ya kunyonga

86566 Mahakamapic Mahakama yaiamuru Tanzania kufuta adhabu ya kunyonga

Sun, 1 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHRP) imeiamuru Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho katika sheria ya kanuni za adhabu ili kuondoa sharti la lazima la adhabu ya kunyongwa kwa washtakiwa wanaopatikana na hatia katika kesi za mauaji.

Kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni za adhabu (Penal Code –PC), mtu anayepatikana na hatia katika kesi za mauaji, adhabu yake ni moja tu yaani kunyongwa na haina mbadala.

Hata hivyo, mahakama hiyo imesema sharti la lazima la adhabu ya kunyonga inakiuka haki ya kuishi inayolindwa na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ambao Tanzania imeuridhia na kuusaini.

Pia mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha imesema utekelezaji wa adhabu hiyo ya kifo kwa kunyonga hukiuka haki ya utu.

Hivyo Mahakama imeipa Serikali ya Tanzania mwaka mmoja kuifanyia marekebisho sheria hiyo kwa kuondoa sharti la lazima la adhabu ya kunyongwa kama ilivyo sasa.

Marekebisho hayo kwa mujibu wa Mahakama hiyo yanalenga kuzipa mahakama nchini mamlaka ya kupima na kutoa adhabu kulingana na mazingira maalumu, tofauti na zilivyo sasa zilivyofungwa mikono na hazina mamlaka ya kuamua vinginevyo. Mahakama hiyo imetoa amri hizo kwa Serikali ya Tanzania katika hukumu yake ya kesi ya kumbukumbu iliyofunguliwa na Watanzania watano; Ali Rajabu na wenzake wanne waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rajabu na wenzake; Angaja Kazeni maarufu kama Oria, Geofrey Stanley ‘Babu’, Emmanuel Michael ‘Atuu’ na Julius Petro walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu mwaka 2011 baada ya kupatikana na kosa la mauaji.

Rajabu na wenzake hao ambao kwa sasa wamefungwa katika gereza kuu la Arusha, walikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini wakashindwa na licha ya mahakama hiyo kubaini kasoro za kisheria katika hukumu ya Mahakama Kuu, ilizirekebisha na kuidhinisha adhabu hiyo.

Katika shauri hilo la maombi namba 007 la mwaka 2015, walikuwa wakidai kuwa pamoja na mambo mengine waliyodai kuwa ni haki zao zilizokiukwa na mahakama za ndani pia walikuwa wakipinga adhabu ya kunyongwa wakidai inakiuka haki yao ya kuishi na utu.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Serikali ilitetea adhabu hiyo kwamba ipo kwa mujibu wa sheria zake na kwamba iko sawasawa na kanuni za kimataifa ambazo hazizuii utolewaji wa adhabu hiyo.

Mahakama katika hukumu yake, imetupilia mbali utetezi wa Serikali, badala yake imekubaliana na hoja za wadai kuwa adhabu hiyo kwa jinsi ilivyo katika sheria za Tanzania inapora haki ya kuishi kwa lazima na kwamba jinsi inavyotekelezwa hukiuka haki ya utu.

Hivyo imesema Serikali kwa kuwa na sheria hiyo inakiuka ibara ya 4 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

Licha ya kukubali kuwa adhabu hiyo hutolewa kwa mujibu wa sheria za nchi na kwamba hutolewa na mahakama zenye mamlaka, lakini utaratibu wa kufikia adhabu hiyo si wa kisheria kwani si wa haki.

wa utaratibu wa kisheria si tu unahusisha haki za mwenendo wa shauri bali pia haki zinazohusiana na mchakato wa utoaji adhabu, hasa mamlaka ya mahakama kuzingatia mazingira maalum ya mshtakiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz