Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yahoji upande wa mashtaka upelelezi kesi ya kina Mwanyika ulipofikia

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeutaka upande wa mashtaka kwenye kesi ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya Dola za Marekani milioni 112 dhidi ya aliyekuwa rais wa Migodi ya Pangea, North Marathas exploration na Bulyanhulu, Deogratius Mwanyika na wenzake waeleze upelelezi wa kesi hiyo, umefikia hatua gani.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina amesema hayo leo Mei 17,2019 baada ya Wakili wa Serikali, Wankyo Simon kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika wanasubiri taarifa kutoka nje ya nchi walikoomba msaada.

Wakili wa utetezi, Gasper Nyika ameomba upande wa mashtaka ueleze bado muda gani upelelezi huo kukamilika kwa sababu  mara kwa mara wamekuwa wakisema upelezi bado na ni maeneo gani hawajayakamilisha na kwanini hawayataji?

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, mwaka huu na kuutaka upande wa mashtaka siku hiyo kuja na majibu ya upelelezi ulipofikia.

Mbali na Mwanyika, washtakiwa wengine  ni Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo,  Mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku, Assa Mwaipopo, Kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 39 ya utakatishaji na kukwepa kodi ya zaidi ya Dola za Marekani 112 milioni.

Pia Soma

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, mashtaka saba ya kughushi, mashtaka 17 ya utakatishaji wa fedha, kuwasilisha nyaraka  za uongo  kwa  Mamlaka ya Mapato Tanzanian (TRA), shitaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka manane ya kukwepa kodi na shtaka moja la kutoa rushwa.

Washitakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30,2007 katika sehemu tofauti za Jiji la Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maeneo mengine ambayo washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo ni katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na nchini  Uingereza.

Aidha mshtakiwa Mwanyika  na Lugendo, wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa kamishna Generali wa TRA huko Biharamulo kwa nia ya kukwepa kulipa kodi ya Dola za Marekani 9,309,600 ambayo ilikuwa ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha Dola za Marekani 374,243,943,45 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

Pia, wanadaiwa kati ya Novemba 2,  2012 na Novemba 27, 2015 huko Shinyanga walitoa Rushwa ya Sh 718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye  ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kughushi, washtakiwa hao wanadaiwa kwa nia ya ulaghai, waligushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30, 2014 Kampuni ya Pangea limited ilikubali kukopa Dola za Marekani 90,000,000 ikiwa na riba kutoka benki ya kimataifa ya Barrick huku wakijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la kutoa nyaraka ya uongo, mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30, 2018 huko BOT iliyopo Wilaya ya Ilala, kwa makusudi aliwasilisha  nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya kampuni ya mgodi wa Bulyanhulu na Barrick international bank Corp kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, kati ya June, 2001 na Desemba 13, 2007, Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa USD 416,100,000 kutoka Barrick.

Chanzo: mwananchi.co.tz