Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yagomea ombi la ZAS

Mahakama Kuu 2 MUDA HUU Mahakama yagomea ombi la ZAS

Fri, 13 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya ZAS Investment Company Limited, ya kuhamisha kesi inayoikabili kutoka kwa Jaji Edwin Kakolaki, kwenda kwa Jaji Butamo Philip.

Baada ya kutupilia mbali maombi hayo ya kampuni hiyo, mahakama hiyo imeamua kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo katika hatua ya pingamizi la awali lililowekwa na kampuni hiyo dhidi ya shauri linaloikabili mahakamani hapo lililofunguliwa na benki ya Equity.

Katika shauri hilo la maombi namba 513, benki hiyo inayowakilishwa na wakili Shalom Msakyi wa kampuni ya Lior Attorney.

Benki hiyo inaiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuifunga kampuni hiyo kutokana na kushindwa kulipa deni la pesa ambazo inaidai jumla ya Sh22 bilioni.

Kwa mujibu wa hati ya maombi, benki hiyo inaidai kampuni hiyo Dola za Marekani 8.69 milioni na Sh73 milioni, zikiwa ni mkopo ambao iliipatia kampuni hiyo kwa ajili ya ujenzi kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2017.

Kwa mujibu wa hati hiyo, deni hilo ni pamoja na riba.

Kufuatia shauri hilo, kampuni hiyo imewasilisha pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo ilitupilie mbali shauri hilo huku ikitoa hoja sita, zinazoeleza kuwa shauri hilo halistahili kuwepo mahakamani hapo.

Sambamba na pingamizi hilo la awali, shauri hilo lilipotajwa kwa mara ya kwanza tarehe Oktoba 4, 2023, ndipo Wakili wa kampuni hiyo Frank Mwalongo alipoomba shauri hilo lihamishwe kutoka kwa Jaji Kakolaki kwenda kwa Jaji Philip.

Katika maombi hayo wakili Mwalongo alidai kuwa anaomba shauri hilo lihamishiwe kwa Jaji Philip kwa kuwa kuna shauri lingine kama hilo la mteja wake mwingine (kampuni ya Continental Reliable Clearing (T) Limited).

Pia, wakili Mwalongo aliomba mahakama hiyo itoe amri kuielekeza benki hiyo isitoe matangazo magazetini kuhusiana na maombi yake ya kutaka kampuni hiyo ifungwe, kama sheria inavyoelekeza.

Wakili wa benki hiyo, Shalom Msakyi alipinga maombi na hoja za Wakili Mwalongo zilizo omba kuhamishwa kwa kesi hiyo.

Wakili Msakyi alidai kuwa shauri lililopo kwa Jaji Philip ni tofauti na kwamba shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Kakolaki halitokani na shauri lililopo kwa Jaji Philip.

Pia alidai kuwa Jaji Kakaolaki anao uwezo wa kusikiliza shauri hilo.

Kuhusu amri ya kusitisha kutoa matangazo ya kampuni hiyo kutaka kufungwa, Wakili Msakyi alidai hoja ya Wakili Mwalongo haina mashiko, kwani sheria ya ufilisi inamtaka atangaze kwenye gazeti maombi hayo ndani ya siku 7 baada ya kumpatia nakala mjibu maombi.

Mahakama katika uamuzi wake, Oktoba 11, 2023 iliamua kutupilia mbali maombi ya kuhamisha file kwenda kwa Jaji Phillip na kuamua kuendelea na usikilizwaji shauri hilo kuanzia pingamizi hilo.

Jaji Kakolaki alipanga kusikiliza pingamizi hilo kwa njia ya maandishi, ambapo alielekeza mjibu maombi (ZAS) kuwasilisha hoja zake za ufafanuzi wa pingamizi lake Oktoba 26, na mwombaji (Equity Bank), kuwasilisha majibu ya hoja hizo za ZAS Novemba 7, mwaka huu.

Katika pingamizi hilo kampuni hiyo inadai kuwa shauri hilo la maombi ya kufungwa kwake halistahili kutokana na kutokutaja kifungu cha sheria kinachoipa mamlaka mahakama na kwamba hakuna maazimio ya bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo kufungua shauri hilo.

Pia kampuni hiyo inadai kuwa shauri hilo halina maana bali ni matumizi mabaya ya taratibu za mahakama, kwamba lina dosari kubwa za kisheria zisizorekebishika.

Vilevile inadai kuwa hati ya kiapo ina kasoro katika sehemu ya uthibitisho kwa kuonesha kuwa kuna waombaji wawili wakati kwenye hati ya maombi ni mwombaji mmoja tu na kwa mtoa kiapo kutoa uthibitisho wakati anajitambulisha kuwa ni Mkristo.

Pia Jaji Kakolaki alipanga shauri la msingi kutajwa Desemba 6 mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live