Idadi kubwa ya wakazi wa jiji la Arusha wamejitokeza leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi, kusikiliza hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na wenzake wawili.
Watu wameanza kufika saa mbili asubuhi, Sabaya na wenzake wamefikishwa mahakamani hapo saa 3:05 asubuhi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo Oktoba Mosi, 2021 baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, kutokamilisha kuandika hukumu hiyo.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Amworo ameshafika mahakamani hapo na muda mfupi ujao hukumu itaanza kusomwa.
Agosti 12 watuhumiwa hao walielezwa kuwa wana kesi ya kujibu baada ya kukamilika ushahidi wa mashahidi 11 wa Jamhuri na vielelezo vinane.
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na mawakili Dancan Oola, Mosses Mahuna, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka, Fridolin Gwemelo na Jeston Jastin.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Abdallah Chavula na mawakili wa serikali Felix Kwetukia na Baraka Mgaya.