Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaeleza Mbowe, Matiko walivyokiuka masharti ya dhamana

28473 Mahakama+pic TanzaniaWeb

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Leo Ijumaa Novemba 23, 2018 Mahakama ya Hakimu  Mkazi Kisutu imewafutia dhamana mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amesema kitendo kilichofanywa na washtakiwa hao ni kudharau amri za mahakama kwa makusudi.

Kuhusu Mbowe amesema sababu zilizotolewa na mdhamini wa mwenyekiti huyo wa Chadema kuwa Novemba 8, 2018 aliugua ghafla na kupelekwa nje ya nchi akiwa mahututi, huku wakili wake  akieleza kuwa Mbowe alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, ni za  uongo kwa sababu zinakinzana na taarifa alizotoa mshtakiwa mwenyewe.

Amesema katika maelezo yake Mbowe alisema kuwa alisafiri nchini Oktoba 28, 2018 kuelekea Washington DC Marekani kuhudhuria mkutano wa Oktoba 30 na kwamba Oktoba 31, 2018 usiku alipotaka kusafiri kurejea Tanzania kwa ajili ya kusikiliza kesi yake aliugua ghafla.

Amesema Mbowe alieleza kuwa baada ya kushambuliwa na ugonjwa, alishauriwa asisafiri umbali mrefu kwa ndege lakini kutokana na hati yake ya kusafiria kuonyesha alisafiri umbali mwingine mrefu kwa ndege, inaonyesha kwamba alikuwa anadharau amri za mahakama kwa makusudi.

Kuhusu Matiko, Hakimu Mashauri amesema Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa sheria,  na sheria inamtaka mshtakiwa yeyote pamoja na cheo chake kutambua kuwa yupo sawa na watu  wengine wanyonge, hivyo bado anatakiwa kutimiza amri za mahakama.

Amesema sababu alizozitoa Matiko kuwa alihudhuria ziara ya kibunge nchini Burundi si za msingi na hazikidhi matakwa ya kutofika mahakamani.

Amebainisha kuwa kutokana na kilichofanywa na washtakiwa hao, amewafutia dhamana.

Baada ya uamuzi huo, wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala alitoa taarifa kwa kuieleza mahakama kuwa wataukatia rufaa uamuzi huo Mahakama Kuu.

Baada ya Kibatala kueleza hayo, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai kuwa hoja zilizowasilishwa na  Kibatala za kuomba ahirisho zinakosa msingi wa kisheria na hata kiutaratibu.

Nchimbi amedai kuwa hoja hiyo kimsingi haina mashiko, na kuhusu kukata rufaa mahakama imekwishatoa maamuzi kutokana na mwenendo wa shauri hilo.

Soma zaidi:

VIDEO: Mbowe, Matiko wanyimwa dhamana, sasa kulala mahabusu



Chanzo: mwananchi.co.tz